CAR-USALAMA

Mapigano makali yazuka mjini Bangui

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa karibu na eneo jirani la kata ya PK5 mjini Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa karibu na eneo jirani la kata ya PK5 mjini Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. REUTERS/Siegfried Modola

Nchini Jmahuri ya Afrika ya Kati, mapigano makali yalitokea Jumapili jioni Oktoba 30 katika kitongoji cha PK5 mjini Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa vyanzo rasmi, makundi matatu ya wanamgambo yalipambana. Angalau watu kumi, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa kundi moja waliuawa, na wengine wengi kujeruhiwa. 

Matangazo ya kibiashara

Jumapili, Oktoba 30 kwenye saa 11:30 (saa za nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati) na kwa muda wa zaidi ya saa moja, milio ya risasi ilisikia katika kitongoji cha PK5, kitongoji wanakoishi Waislamu wengi. Chanzo cha Umoja wa Mataifa kimethibitisha kuwa zilisikika bunduki aina ya RPG.

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, makabiliano hayo yalikua kati ya makundi ya wanamgambo ya Mohammed Ali Fadul na mawili yanayoongozwa na Kapi Issa, almaarufu 50-50, na Abdul Danda, anayetuhumiwa kutekeleza mauaji ya kiongozi wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati (Faca), Marcel Mombeka, mapema mwezi huu. Mauaji ambayo yalisababisha ulipizaji kisasi na kuzuka kwa ghasia, ambapo watu kadhaa waliuawa.

Haijajulikana bado sababu sahihi ya makabiliano haya, lakini kwa mujibu wa chanzo cha Umoja wa Mataifa, huenda ni kutokana na "kutoelewana" kati ya makundi hayo tofauti. Lakini haijajulikana nani alianza kushambulia mwengine na kwa nini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wakazi kadhaa wa kitongoji hiki waliohojiwa kwa simu na RFI, hali ya utulivu inaonekana kurejea tangu baada ya makabiliano hayo kumalizika. Lakini wakazi wa kitongoji cha PK5 wamesalia nyumbani kwa uoga na hofu ya kuzuka kwa mapigano mapya. Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (Minusca) kimetuma askari wake katika kitongoji hiki.