ICC-AFRICA-UN

Afrika yaendelea kugawanyika kuhusu kujitoa ICC, mjadala mkali waendelea UN

Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC.
Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC. REUTERS/Jerry Lampen/File Photo

Mgawanyiko kuhusu kujitoa kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC kwa nchi za Afrika, hivi sasa unashuhudiwa dhahiri, hali iliyoshuhudiwa wakati wa mjadala wa kupokea ripoti ya mwaka kuhusu mahakama hiyo kwenye baraza la umoja wa Mataifa, UNSG.

Matangazo ya kibiashara

Nchi nyingi kutoka bara la Ulaya, Asia Pacific na Latin America, zilipata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimeungana na mataifa hayo kuonesha uungaji mkono wa nchi kuendelea kusalia kwenye mahakama hiyo.

Nchi kadhaa za dunia zimeeleza kusikitishwa na uamuzi wa hivi karibuni wa baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Burundi na Gambia, kutangaza kujitoa kwenye mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama ya ICC.

Licha ya Afrika Kusini kutokutuma mjumbe wowote kwenye mjadala huo, suala lake la kuamua kujitoa lilijadiliwa kwa kina na nchi wanachama zilizohudhuria.

Wakati wa mjadala huo, nchi ya Kenya imesema kuwa ripoti iliyowasilishwa imeshindwa kuelezea na kutatua masuala mtambuka ambayo yamezifanya baadhi ya nchi za Afrika kuamua kujitoa kwenye mahakama hiyo.

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda, 14 November 2013 .
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda, 14 November 2013 . UN Photo/Eskinder Debebe

Mjumbe wa wizara ya mambo ya nje wa Kenya, Thomas Amolo, ameitaka mahakama hiyo kushtuka na kuchukua hatua kutatua mapungufu yaliyojitokeza ikiwa inataka nchi za Afrika ziendelee kubakia.

Balozi wa Burundi kwenye umoja wa Mataifa, Albert Shigiro, amesema kuwa dunia haipaswi kushangazwa na uamuzi wa baadhi ya nchi za Afrika kuanza kujiondoa kwenye mahakama hiyo, na kwamba wakuu wa mahakama hiyo wajiulize ni kwanini nchi za Afrika zimeamua kuanza kujiondoa sasa na sio wakati mwingine wowote ule, akiituhumu mahakama hiyo kwa kufanya kazi kwa maelekezo kutoka nchi za magharibi.

Hata hivyo wito huu wa Kenya na nchi ya Burundi, ulipingwa vikali na baadhi ya nchi nyingine za Afrika, ikiwemo Botswana, Senegal, Nigeria na Tanzania, nchi ambazo zenyewe zimesema kuwa mazungumzo yanafaa kufanyika na sio nchi hizo kutaka kujiondoa kwa kuwa zinatuma ujumbe mbaya wa kuwalinda wahalifu wa kivita.

Balozi wa Tanzania kwenye umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, amesema kuwa ni wazi kuna masuala ambayo lazima mahakama hiyo iyatatue ikiwa inataka kupata uungwaji mkono wa nchi za Afrika, lakini akasisitiza kuwa, hakuna haja ya kujiondoa kwa sasa kwakuwa masuala yaliyoibushwa hivi karibuni yanaweza kutatuliwa na mahakama ikajenga imani tena kwa nchi hizo.