DRC-SIASA

Baraza kuu la Maaskofu DRC laendelea na majukumu yake

Maaskofu, wajumbe wa Baraza Kuu la Maaskofu nchini DRC (Cenco).
Maaskofu, wajumbe wa Baraza Kuu la Maaskofu nchini DRC (Cenco). cenco.cd

Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeanza upya mchakatao wa kupatanisha wadau wote nchini humo ili kufikia mwafaka wa kitaifa baada ya upinzani ulio na msimamo mkali kutupilia mbali maazimio ya mazungumzo ya kitaifa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa zinazoaminika, Baraza hilo maarufu kama (Cenco) limeombwa na Rais Joseph Kabila mwenyewe mwishoni mwa juma lililopita, liingilie kati ili kusawazisha tofauti zilizopo.

Bila kupoteza muda, Maaskofu wameanza mchakato huo Jumatatu wiki hii kwa kuanzia na viongozi wa upinzani wanaopinga makubaliano ya kisiasa kati ya serikali na wapinzani walio wachache ambao wanamruhusu rais kabila kuendelea kukaa madarakani hadi Aprili 2018 kinyume na Katiba.

Maaskofu wanawataka wadau hao kutozungumzia chochote hadharani na kuwa wa siri, huku sharti la pili likiwa Muungano wa Rassemblement na wa Front pour le respect de la constitution chini ya chama cha MLC waandike hoja zao na kuziwasilisha.

Maaskofu hao hawakuficha wasiwasi wao kuona tofauti kubwa mno baina ya washiriki wa mazungumzo na wengine na kuahidi kuweka mazingira sawa kwa majadiliano zaidi kwa ajili ya uchaguzi wa urais mwaka 2017.