AFRIKA KUSINI

Watu zaidi wajitokeza kushinikiza mwendesha mashtaka Afrika Kusini kujiuzulu

Maaskofu nchini Afrika Kusini, wameingia kwenye orodha ya watu maarufu nchini humo, ambao wanamtaka mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali, Shaun Abrahams, kujiuzulu nafasi yake.

Mwendesha mashtaka wa Serikali ya Afrika Kusini, Shaun Abrahams, picha imepigwa, October 31,2016.
Mwendesha mashtaka wa Serikali ya Afrika Kusini, Shaun Abrahams, picha imepigwa, October 31,2016. REUTERS/Siphiwe Sibeko
Matangazo ya kibiashara

Askofu mstaafu wa kanisa la Anglican, Njongonkulu Ndungane, ameungana na raia, wanaharakati na wanasiasa nchini humo ambao wanashikinikiza Abrahams kuondoka ofisini.

Hatua hii imekuja baada ya ofisi ya mwendesha mashtaka kuondoa mashtaka ya udanganyifu na matumizi mabaya ya ofisi dhidi ya waziri wa fedha Pravin Gordhan pamoja na wafanyakazi wengine wanne wa mamlaka ya mapato nchini humo.

Kwenye taarifa yake askofu Ndungane, amesema kuwa mwendesha mashtaka ni lazima ajiuzulu nafasi yake kwa manufaa ya uma ili kutoa funzo kwa watu wengine ambao wanadharau harakati ngumu za kupigania uhuru wa taifa hilo.

Waziri wa fedha wa Afrika Kusini, Pravin Gordhan, picha ya tarehe 14 Machi 2016, Johannesburg.
Waziri wa fedha wa Afrika Kusini, Pravin Gordhan, picha ya tarehe 14 Machi 2016, Johannesburg. REUTERS/Siphiwe Sibeko

Mwishoni mwa juma pia, chama cha SACP kilitoa wito kwa bunge la nchi hiyo kufanya kikao cha dharura kujadili uwezo wa mwendesha mashtaka Abrahams, kuendelea kusalia ofisini.

Chama hicho kinasema kuwa, uamuzi wa mwendesha mashtaka kuamua kutomfungulia mashataka ya udanganyifu waziri wa fedha, ni uamuzi uliochukuliwa kisiasa kwa malengo ya watu fulani kulindwa.

Abrahams akiongea na wanahabari wakati akitangaza kuondoa mashtaka dhidi ya waziri Gordhan, amesema kuwa haoni kama kuna sababu yoyote ya msingi ya yeye kujiuzulu au kumuomba radhi mtu yoyote.