IVORY COAST

Ivory Coast: Upinzani wapinga matokeo ya kura ya maoni iliyoidhinisha mabadiliko ya katiba

Wasimamizi wa uchaguzi nchini Ivory Coast wakiwa wanahesabu kura hivi karibuni katika kura ya maoni kuidhinisha mabadiliko ya katiba mpya
Wasimamizi wa uchaguzi nchini Ivory Coast wakiwa wanahesabu kura hivi karibuni katika kura ya maoni kuidhinisha mabadiliko ya katiba mpya REUTERS/Luc Gnago

Upinzani nchini Ivory Coast unapinga matokeo ya kura ya maoni yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, kuidhinisha kufanyika mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo, matokeo ambayo upinzani unasema ni ya uongo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara amesema kuwa mabadiliko hayo ni muhimu ili kusaidia kumaliza sintofahamu ya utaifa huku wakosoaji wa Serikali wakiona kura hiyo ni kama maandaliz ya kiongozi huyo kumuandaa mrithi wake wakati muhula wake utakapotamatika mwaka 2020.

Upande uliokuwa unaunga mkono mabadiliko ya katiba, ulishinda kwa asilimia 93 ya kura zote zilizopigwa siku ya Jumapili, lakini cha kushangaza ni kuwa wapiga kura wengi waliokuwa wanastahili kushiriki zoezi hilo waliamua kusalia majumbani baada ya tangazo la upinzani kuwataka watu wasijitokeze kupiga kura.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini Ivory Coast ni asilimia 42 pekee ya wapiga kura ndio waliojitokeza kushiriki kwenye zoezi la kupiga kura mabadiliko ya katiba.

Punde baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, viongozi wa upinzani walijitokeza na kukashifu matokeo hayo waliyosema hayakuwa ya kweli na yalitengenezwa.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyomo kwenye katiba iliyoidhinishwa ni pamoja na kuanzishwa kwa nafasi ya makamu wa rais na baraza la Seneti huku yule makamu wa rais wa tatu akichaguliwa na Rais.