AFRIKA KUSINI

Mahakama kuu Afrika Kusini yaagiza kuchapishwa kwa ripoti ya tuhuma za rushwa dhidi ya Zuma

Waandamanaji wafuasi wa chama cha EFF nchini Afrika Kusini wakiwa nje ya jengo la mahakama kuu ya Afrika Kusini, Novemba 2, 2016.
Waandamanaji wafuasi wa chama cha EFF nchini Afrika Kusini wakiwa nje ya jengo la mahakama kuu ya Afrika Kusini, Novemba 2, 2016. REUTERS/Mike Hutchings

Mahakama kuu nchini Afrika Kusini, imemuagiza mkurugenzi wa ofisi ya mkaguzi wa mali ya uma, kuchapisha ripoti ya tuhuma za rushwa dhidi ya Rais Jacob Zuma, ripoti ambayo huenda ikawa pigo kwa Zuma ikiwa atakuwa amehusishwa kwenye tuhuma za rushwa.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa mahakama umekuja, baada ya Jumatano asubuhi, mawakili wa Rais Zuma kuiambia mahakama kuwa, mteja wao ameamua kuondoa pingamizi lililokuwepo mahakamani kuzuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

Ripoti hiyo sasa, inatakiwa kuchapishwa kabla ya saa kumi na moja kamili za jioni ya Jumatano ya Novemba 2 kwa saa za Afrika Kusini, ambapo itakuwa ni saa 6 kamili jioni kwa saa za Afrika ya Kati.

Uamuzi wa mahakama umekuja, wakati huu maelfu ya waandamanaji wakiwa wamekusanyika kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Pretoria kushinikiza Rais Zuma kuondoka madarakani.

Ripoti ya mkaguzi wa mali ya uma inahusu uchunguzi uliofanywa kuhusu uhusiano alio nao Rais Zuma na familia ya kihindi ya Gupta, ambapo anadaiwa kuwa familia hiyo imekuwa ikimchagulia baadhi ya mawaziri.

Akisoma uamuzi wa mahakama, jaji kiongozi kwenye kesi hiyo, Dustan Mlambo, amesema "Mkaguzi mkuu wa mali za uma anaagizwa kuitoa ripoti hiyo sio zaidi ya saa kumi na moja jioni."

Aliyekuwa mkaguzi mkuu wa mali za uma, Thuli Mandonsela, alimaliza kuandika ripoti yake mwezi mmoja uliopita kuhusu uhusiano wa familia ya Gupta na Rais Zuma, siku chache tu kabla ya muda wake kuhudumu ofisini kutamatika.

Ripoti hii ilikuwa ichapishwe October 14 lakini Rais Zuma alienda mahakama kuzuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

"Leo ni siku ya kihistoria...Jacob Zuma lazima awajibishwe," alisikika akisema kiongozi wa chama cha upinzani cha DA, Mmusi Maimane, ambaye pia amepongeza uamuzi wa mahakama kuu.

Rais Zuma ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 74, mpaka sasa amefanikiwa kushinda mara kadhaa kura ya kutokuwa na imani nae bungeni, lakini amekuwa akikabiliwa na ukosolewaji mkubwa kuhusu utawala wake na tuhuma za rushwa dhidi yake.