UNMISS-KENYA

UN yaziba nafasi ya Luteni Ondieki Sudan Kusini

Sehemu ya kikosi cha wanajeshi wa China ambao wanahudumu nchini Sudan Kusini, 27 February 2015.
Sehemu ya kikosi cha wanajeshi wa China ambao wanahudumu nchini Sudan Kusini, 27 February 2015. UN Photo/JC McIlwaine

Siku chache baada ya katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kumfuta kazi kamanda wa vikosi vya kulinda amani nchini Sudan Kusini, umoja huo umemteua afisa wa jeshi la China kukaimu nafasi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jumanne ya tarehe 1, katibu mkuu Ban Ki Moon, aliagiza kuondolewa kwenye nafasi yake Luten Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki kutoka Kenya, aliyekuwa akiongozi vikosi vya kulinda amani humo, siku chache baada ya kupokea ripoti iliyokosoa utendaji kazi wa vikosi hivyo.

Ripoti iliyowasilishwa kwa katibu mkuu, ilieleza kwa kina namna ambavyo vikosi vya UNMISS vilishindwa kabisa kutoa usalama kwa raia wakati mapigano yalipozuka jijini Juba mwezi Julai mwaka huu, ambapo pia makao yake makuu jijini Juba yalishambuliwa.

Taarifa ya katibu mkuu Moon, imesema kuwa, nafasi ya Luteni Jenerali Ondieki inakaimiwa na Meja Jenerali Chaoying Yang, ambaye alikuwa ni naibu kamanda wa Ondieki.

Meja Yang hata hivyo hakuwa akihudumu kama kamanda wa vikosi vya China ambavyo vilitajwa kwenye ripoti ya uchunguzi, ambayo iliwataja askari wake kukimbia maeneo yao ya lindo.

Nchi ya Kenya ilikataa kupendekeza jina la kamanda mwingine kuziba nafasi ya Ondieki, na hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje.

Baada ya uamuzi huo, Serikali ya Kenya ilijibu hatua ya katibu mkuu Moon, kwa kuagiza kuondoka kwa wanajeshi wake elfu moja nchini Sudan Kusini ambao wanahudumu kwenye tume ya UNMISS.