MABADILIKO TABIA NCHI-MARRAKESH

Mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wang'oa nanga mjini Marrakech

Msemaji wa tume ya umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, UNFCCC, Nick Nuttall, Marrakech, Morocco, November 6, 2016.
Msemaji wa tume ya umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, UNFCCC, Nick Nuttall, Marrakech, Morocco, November 6, 2016. REUTERS/Youssef Boudlal

Wakati mjadala mkubwa duniani ukiwa ni uchaguzi mkuu wa urais nchini Marekani juma hili, mataifa duniani yanakutana mjini Marrakech, Morocco kujadiliana na kuanza utekelezaji wa mkataba wa kihistoria wa mabadiliko ya tabia nchi uliotiwa saini jijini Paris, Ufaransa mwaka uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Mkataba huu ambao umeanza rasmi kutekelezwa, ni mkataba wa kwanza unaozitaka nchi za dunia, tajiri na masikini, kuzuia hali ya ongezeko la joto duniani, inayosababishwa hasa na uchomaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi.

"Sasa ni ramani iliyowazi katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi," amesema Manuel Pulgar-Vidal, waziri wa zamani wa mazingira wa nchi ya Peru pamoja na mkuu wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka shirika la WWF.

Lakini wakati huu wapatanishi zaidi ya elfu 15, wakurugenzi watendaji na wanaharakati kutoka nchi 196 duniani, wanakutana mjini Marrakech kwa siku 12 za mazungumzo yanayosimamiwa na umoja wa Mataifa, huku macho na masikio yako kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani, huku mgombea wa Republican Donald Trump akionekana kuukashifu mkataba huu.

Linapokuja suala la hali ya ongezeko la joto duniani, hatari ni kubwa zaidi, alionya rais wa Marekani, Barack Obama.

"Hatua zote tulizopiga kuhusu mabadiliko ya tabia nchi" ikiwemo makubaliano ya Paris yaliyochukua miongo kadhaa ya mazungumzo "uko kwenye sanduku la kura," vyombo vya habari vimegusia vikihusisha na uchaguzi wa Marekani.

Wataalamu wanasema kuwa mgombea wa Republican hawezi kutoa vitisho akidai kuwa atafuta makubaliano ya Paris wakati huu sintofahamu bado ikiendelea kutanda kuhusu utekelezaji wake.

Kwa upande wake mgombea wa Democratic Hillary Clinton ameapa kulinda na kutekeleza yale yaliyokubaliwa na rais Barack Obama kuhusu masuala ya sera za nishati na makubaliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mjini Marrakech, wanadiplomasia wa kimataifa wanajukumu la kuhakikisha wanajifunga mkaja na kumaliza sintofahamu zinazozunguka mkataba wa Paris kuhusu mafanikio yake na kushindwa kwake.

Mpatanishi mkuu wa Ufaransa kuhusu mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi, Laurence Tubiana, amesema kuwa mazungumzo ya wakati huu ni muhimu katika kutamatisha andiko lenyewe wakati utekelezaji ukiendelea.