MAREKANI-SIASA

Uchaguzi wa Marekani wakosa msisimko kwa Waafrika kinyume na ilivyokuwa mwaka 2008

Donald Trump na Hillary Clinton wagombea wa urais nchini Marekani
Donald Trump na Hillary Clinton wagombea wa urais nchini Marekani REUTERS/Carlo Allegri/ Brian Snyder

Raia wa Marekani wanapojiandaa kupiga kura siku ya Jumanne kumchagua rais mpya atakayewaongoza kwa muda wa miaka minne ijayo, kipindi hiki siasa za Marekani hazijafuatiliwa kwa karibu sana kama ilivyokuwa mwaka 2008 wakati rais Barrack Obama alipokuwa anatafuta uongozi wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Raia wa Marekani wanapojiandaa kupiga kura siku ya Jumanne kumchagua rais mpya atakayewaongoza kwa muda wa miaka minne ijayo, kipindi hiki siasa za Marekani hazijafuatiliwa kwa karibu sana kama ilivyokuwa mwaka 2008 wakati rais Barrack Obama alipokuwa anatafuta uongozi wa nchi hiyo.

Mwaka 2008, ushindi wa Obama ulikuwa kama ndoto iliyokuwa imetimia kwa Marekani kupata mtu mweusi kuongoza nchi hiyo yenye nguvu duniani tena aliye na mizizi barani Afrika.

Mfano mzuri ni nchini Kenya, wakati Obama aliposhinda Uchaguzi, vichwa vya Habari katika Magazeti ya nchi hiyo yaliandika, “Mtoto wetu, tumaini letu”.

“Obama alituwakilisha sisi kama Waafrika, aliishi hapa nchini Kenya, maisha ya kawaida na hata kupanda matatu,” amesema Brian Wanyama Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kibabii na mchambuzi wa siasa za Kimataifa.

Mwaka huo raia wa Kenya walimpiga kura ya bandia Obama na kumtangaza mshindi.

Obama alipotangazwa mshindi, serikali ya Kenya ilitangaza siku moja ya mapumziko ili kuruhusu Wakenya kusherehekea ushindi huo.

“Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kwa Mwafrika, aliye na mizizi barani Afrika kuwania urais, ulikuwa ni wakati wa kipekee, baba yake alikuwa ni raia wa Kenya hali iliyoleta furaha kubwa sana,” amesisitiza Wanyama.

Wanyama anaona kuwa, wakati huu siasa za Marekani haziwavutii sana waafrika kwa sasa, watu wengi wanahisi kuwa wagombea wa sasa ni Wazungu na hivyo hawana uhusiano wa karibu na waafrika kama ilivyokuwa kwa Obama.

Brian Wanyama uchambuzi siasa za Marekani Novemba 7 2016

 

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack Obama AFP/Jose Luis Magana

Hata hivyo, miaka minane baadaye, bara la Afrika linahisi halijanufaika sana na uongozi wa rais Obama kinyume na matarajio waliyokuwa nayo wakati akiingia madarakani.

Obama atakumbukwa kuzuru nchi ya Senegal, Afrika Kusini na Tanzania mwaka 2013 na baadaye Ethiopia na Kenya mwaka 2015 ziara ambayo wengi wanaona kuwa hawajaona manufaa ya ziara hiyo.

Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa rekodi ya rais Obama barani Afrika ikilinganishwa na ya mtangulizi wake George W Bush ni ndogo sana licha ya uongozi wake kuzindua mradi wa Power Africa mwaka 2013, kuhakikisha kuwa mataifa mengi ya Afrika yanapata umeme.

"Wagombea wote wawili hawajaonesha kile ambacho wanakisimamia kuhusu maswala ya bara la Afrika," alisema Abdulkarim Atiki mchambuzi wa siasa za Kimataifa akiwa jijini Dar es salaam.

"Trump amekuwa akitoa matamshi mazito kuhusu maswala ya viongozi wanaoendelea kukaa madarakani lakini mwenzake Clinton pamoja na kuwa na uzoefu wa kisiasa, hajaonesha ni kwa namna gani atalisaidia bara hili kuendelea kisiasa na kupata maendeleo," ameongezea Atiki.

Abdulkarim Atiki mchambuzi wa siasa akiwa jijini Dar es salaam Novemba 6 2016

Mradi huu unalenga kuwanufaisha watu Milioni 600 kupata umeme na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa nishati kwa Megawatts 30,000 na tayari serikali ya Marekani imetoa Dola Bilioni 7 kufanikisha mradi huu kwa muda wa miaka mitano.

Uongozi wa Bush, utakumbukwa sana kwa kuanzisha mradi wa PEPFAR kununua dawa kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na kusaidia kuokoa maisha ya Mamilioni ya watu waliokuwa wameathirika.

Pamoja na hili, wakati wa Bush, uongozi wake ulisaidia kumaliza machafuko barani Afrika katika hasa katika mataifa ya Sudan, Congo, Angola, Liberia, Sierra Leone lakini Obama anakaribia kuondoka akiacha mzozo wa Sudan Kusini na Somalia.

Kuelekea Uchaguzi wa Marekani, Waafrika wengi hawafahamu hatima yao hasa ikiwa Trump atashinda kwa sababu hana uzoefu wa kisiasa na hajaweka wazi sera yake ya mambo ya nje hususan ya Afrika.

Donald Trump na Hillary Clinton wagombea urais nchini Marekani
Donald Trump na Hillary Clinton wagombea urais nchini Marekani REUTERS/Carlos Barria

Trump amekuwa akisema kuwa akiwa rais, idadi ya Waislamu wanaokwenda Marekani itapunguzwa, Mexico itajenga ukuta katika mpaka wake na Marekani lengo ni kudhibiti wahamiaji wanaokwenda Marekani wakiwemo watu kutoka barani Afrika.

Je, Trump akiwa rais mradi wa rais Obama anayemaliza muda wake wa Power Africa utaendelea kuwepo ? Ni swali kubwa linalowasumbua Waafrika.

Hata hivyo, Bi. Clinton kutokana na uzoefu wake kama Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Waafrika wengi wana imani kidogo kwa sababu huenda akaendeleza sera za rais Obama.