SIASA-MAREKANI

Viongozi mbalimbali wampogeza Trump kwa kushinda urais nchini Marekani

Viongozi mbalimbali wa dunia wamekuwa wakimpongeza Donald Trump kwa kushinda Uchaguzi wa urais nchini Marekani licha ya kupata ushindi ulioishangaza dunia.

Mmoja wa wafuasi wa Trump wakisherehekea ushindi
Mmoja wa wafuasi wa Trump wakisherehekea ushindi REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Tanzania John Magufuli amempongeza Trump kwa ushindi huo na kusema nchi yake itashirikiana na serikali yake.

“Hongera rais mteule Donald Trump, na watu wa Marekani. Tanzania na mimi tunakuhakikishia kuwa tutandelea na urafiki na ushirikiano ambao tumekuwa nao,” ameandika rais Magufuli katika ukurasa wake wa Twitter.

Ujumbe kama huo pia umetoka kwa rais wa Burundi Piere Nkurunziza.

“Bwana Trump, kwa niaba ya watu wa Burundi, tunakupongeza sana. Ushindi wako ni ushindi wa Wamarekani wote,” aliandika rais Nkurunziza katika ukurasa wake wa Twitter.

Naye rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema anatarajia kufanya kazi na Trump kama ilivyoshirikiana na marais waliopita.

“Nampongeza Donald Trump kwa kuchaguliwa rais wa Marekani.Nitashirikiana naye kama nilivyofanya na viongozi waliomtangulia,” aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Nchini Kenya, hakuna shamrashamra zilizoshuhudiwa kama ilivyokuwa mwaka 2008 na 2012 wakati Barrack Obama alipoibuka mshindi.

Siku Jumanne katika kijiji cha Kogelo Magharibi mwa nchi hiyo anakotokea baba yake Obama, wakaazi wa kijiji hicho walipiga kura ya mwigo na kumpa ushindi Bi.Clinton lakini, matokeo nchini Marekani yamekuwa tofauti.

Wakenya wengi wanahisi kuwa, Wamarekani wamewaangusha katika Uchaguzi huu kwa kushindwa kumchagua Bi.Clinton kuendeleza kazi ya rais Obama ambaye wanasema ni mtoto wao kwa sababu baba yake alikuwa ni Mkenya.