DRC-UNSC

Serikali ya DRC yatakiwa kuheshimu haki ya kuandamana na kufungulia mitambo ya RFI

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalozuru nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umeitaka serikali ya Kinshasa kuheshimu haki ya kuandamana lakini pia kufungulia mitambo ya Idhaa ya Kifaransa ya RFI.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nebula.wsimg.com
Matangazo ya kibiashara

Wito huu umetolewa kwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila baada ya kukutana na ujumbe huo kuzungumzia hali ya kisiasa na usalama nchini humo.

Baada ya mazungumzo ya saa moja na nusu, wajumbe hao kutoka nchi 15 wamesisitiza pia umuhimu wa mazungumzo ya kisiasa nchini humo yanayowashirikisha wanasiasa na wadau wote ili mwafaka wa kisiasa umepatikane na kuungwa mkono na kila mmoja.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe hao, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa François Delattre, amesema vyombo vya usalama nchini humo vina jukumu la kuhakikisha kuwa usalama unakuwepo na unaheshimu haki za raia wa kawaida wanaoikosoa serikali.

Pamoja na hili, Delattre ameongeza kuwa amemwambia rais Kabila ahakikishe kuwa kuna ukabidhianaji wa madaraka kwa njia ya amani pindi tu kipindi chake kitakochomalizika.

Serikali ya Kinshasa imekuwa ikiishtumu RFI kwa kochochea hali ya kisiasa nchini humo baada ya kutokea kwa maandamano ya upinzani miezi miwili iliyopita kushinikiza kujiuzulu kwa rais Kabila muda wake utakapomalizika mwezi Desemba, na kusababisha vifo vya waandamanaji na wengine kukamatwa.

Kinshasa inasema inataka mazungumzo ili kupitia upya mkataba wake na RFI kabla ya kufugulia tena mitambo yake.

Nalo Shirika la kutetea haki za Binadamu la Human Rights Watch, limekuwa likiishtumu serikali ya rais Kabila kwa kuendeleza rekodi ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwakamata wafuasi wa upinzani na kuwazuia.

Mazungumzo ya kisiasa ambayo yalifanyika hivi karibuni na kususiwa na baadhi ya wanasiasa wakuu wa upinzani yamependekeza uchaguzi mpya wa DRC ufanyike mwaka 2018.