MARRAKECH-AFRIKA-TABIA NCHI

COP22: Viongozi wa Afrika wakutana Marrakech, kutoka na kauli moja mwisho wa mkutano

Baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wengine wa dunia, kwenye mkutano wa COP22.
Baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wengine wa dunia, kwenye mkutano wa COP22. REUTERS/Youssef Boudlal

Viongozi kutoka nchi 30 za Afrika, wamekutana mjini Marrakech, Morocco, kando na mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi, COP22, mkutano unaolenga kutaka kulinda maslahi ya bara la Afrika linalokabiliwa na ongezeko kubwa la joto.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huu mkutano wa 22 wa mabadiliko ya tabia nchi ukiwa umeshika kasi nchini Morocco, mkutano huu wa wakuu wa nchi za Afrika, kwa wa waandaaji wake, wanasema kuwa unalenga kujadili njia mpya za kuchukua kukabili ongezeko la joto duniani, pamoja na kujenga mpango wa maendeleo endelevu kwa bara hilo.

Akizungumza hapo jana, mfalme Mohammed wa 6 wa Morocco, amewaambia wajumbe zaidi ya 180 na mawaziri wanaohudhuria mkutano wa COP22 kuwa "hatua iliyofikia sasa hakuna kurudi nyuma hasa katika utekelezaji wa makubaliano ya Paris, yaliyofikiwa mwaka uliopita."

Kwa mataifa ya Kusini, ambayo kwa sasa ndio yako kwenye hatari zaidi ya ongezeko la joto, changamoto iliyopo ni namna gani wanaweza kupata msaada wa haraka wa kifedha na ushauti wa kitaalmu ili kuimarisha uwezo wao na kukabili vilivyo mabadiliko ya tabia nchi.

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande wakati akihojiwa na RFI/ TV5 na France24
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande wakati akihojiwa na RFI/ TV5 na France24

Ikumbukwe kuwa malengo ya nchi zaidi ya 190 zilizoridhia mkataba wa Paris, ni kwa nchi tajiri kuchangia kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kila mwaka hadi kufikia mwaka 2020.

Hata hivyo suala gumu linalosalia sasa kwenye mazungumzo yanyoendelea mjini Marrakech ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa ili kuzifanya nchi zilizoendelea kiviwanda duniani kutoa kiasi hicho cha fedha kwa nchi zinazoendelea.

Wakuu wa nchi za Afrika wamezungumzia pia ni kwa vipi wanaweza kushirikiana wao kwa wao ili kubadilishana teknolojia, utafiti na ubunifu hasa kwenye eneo la teknolojia mbadala zitakazopunguza matumi ya gesi za ukaa.

Mkutano huu wa viongozi wa Afrika, ni muhimu sana hasa kwakuwa watahitaji kuwa na msimamo wa pamoja, ili watakapofikia hatua ya kuanza utekelezaji wa mkataba wa Paris, wawe na sauti moja kueleza msimamo wao.

Wakuu wa nchi zaidi ya 190 wanaokutana kwenye mkutano wa COP22 nchini Morocco wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Wakuu wa nchi zaidi ya 190 wanaokutana kwenye mkutano wa COP22 nchini Morocco wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki kikao hicho ni pamoja na wale kutoka eneo la Sahara ambao ni hasimu wa Morocco, Senegal, Gabon, Ivory Coast na Nigeria, mataifa ambayo yana uhusiano wa karibu na utawala wa Marrakech.

Katika hatua nyingine, akizungumza na idhaa hii katika mahojiano yaliyofanyika kando na mkutano wa Marrakech, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, ameyataka mataifa yote yanayoshiriki, kuhakikisha wanakubaliana na kuanza utekelezaji wa yale yaliyokubaliwa jijini Paris.

Kwa upande wake nae, amesisitiza kuwa hatua iliyofikiwa hivi sasa ni hatua muhimu ambayo nchi hazipaswi kurejea nyuma na badala yake zisonge mbele kuhakikisha dunia inabaki salama.