IVORY COAST-SIMONE GBAGBO

Ivory Coast: Simone Gbagbo agoma kufika mahakamani, yasema itaendelea na kesi bila uwepo wake

Kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu inayomkabili aliyekuwa mke wa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo, Simone Gbagbo, itaendelea bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani, huku maofisa wa mahakama wakimchaguliwa mawakili, amesema rais wa mahakama ya Assize, Jaji Boiqui Kouadjo.

Aliyekuwa mke wa Laurent Gbagbo, Simone Gbagbo, akiwa mahakamani, Juni 30, 2016.
Aliyekuwa mke wa Laurent Gbagbo, Simone Gbagbo, akiwa mahakamani, Juni 30, 2016. ISSOUF SANOGO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Jumatano ya wiki hii, Simone alikataa kufika mahakani sambamba na mawakili wake, ambapo kwenye uamuzi wake Jaji Kouadjo, alisema kesi hiyo inaweza kuendelea bila ya uwepo wake ili kutoa nafasi ya majadiliano kuendelea.

Jaji Kouadjo amechagua jopo la mawakili watakaomuwakilisha na kupanga tarehe nyingine ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kuwa ni Novemba 8.

Kwa mujibu wa barua aliyoiandikia mahakama Jumanne ya wiki hii, Simone Gbagbo alikataa kufika mahakamani Jumatano, barua yake ilisema "sihitaji kuonana na wewe na wala sina haja ya kujua mazungumzo yanahusu nini." ilisema barua yake kwa mahakama.

Mpaka sasa Simone ameshakataa mara kadhaa kutokea mahakamani kwa kile alichokosoa ni kutoonekana kwa mashahidi wanaomtuhumu kuhusika na kuamrisha mauaji dhidi ya waandamanaji.

Simone pia anapinga uwepo wa mashahidi kadhaa kwenye kesi yake kama kiongozi wa kundi la waasi wa zamani wa nchi hiyo, Guillaume Soro, waziri mkuu wa zamani Jeannot Kouadio na na waziri wa zamani Charles Koffi Diby.

Sheria za mahakama kuu nchini Ivory Coast zinamruhusu rais wa mahakama hiyo kuchagua mawakili watakaomuwakilisha mtuhumiwa hata bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.

"Ni yeye mwenyewe ndio amemua kutotokea, tutaendelea bila ya uwepo wake, ameongea kwa kirefu, mawakili wake pia, toka ilipoanza kesi hii May 31," alisema mwendesha mashtaka Aly Yeo.