DRC. MAUAJI-USALAMA

Waandishi wa habari waandamana Mbuji-Mayi baada ya kifo cha mmoja wao

Wakazi wa mji wa Mbuji Mayi waandamana Julai 31, 2006 katika uchaguzi.
Wakazi wa mji wa Mbuji Mayi waandamana Julai 31, 2006 katika uchaguzi. © SCHALK VAN ZUYDAM/AP/SIPA

Marcel Lubala, mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji la serikali la RTNC, aliuawa na watu kadhaa wenye silaha usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne katika mji wa Mbuji-Mayi, katikati mwa DR Congo. Alhamisi hii, waandishi wa habari wenzake walifanya "maandamano ya hasira" wakipinga dhidi ya mazingira ya kazi ya taaluma yao na kuomba haki itendeke baada ya mauaji hayo.

Matangazo ya kibiashara

Huu ni wakati mgumu kwa vyombo vya habari nchini DR Congo. Baada ya hali ya sintofahamu kuhusu sheria inayopiga marufuku vyombo vya habari vinavyorusha matangazo katika ardhi ya nchi hiyo kama haviheshimu masharti yaliyowekwa, mwandishi wa habari wa radio na televicheni ya taifa ya DR Congo, RTNC, aliuawa usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne. Marcel Lubala, mwandishi wa habari wa TRNC katika mji wa Mbuji Mayi, alishambuliwa na watu zaidi ya kumi wenye silaha.

Kutokana na mauaji hayo Waandishi wa habari katika mji wa Mbuji Mayi, mji mkuu wa mkoa wa Kasai-Mashariki, walifanya 'maandamano ya hasira' Alhamisi hii Novemba 17 wakipinga dhidi ya kitendo hicho kiovu alichotendewa Marcel Lubala na hasa maandamano dhidi ya mazongira ya kazi ya taaluma yao. Katika mitaa ya mji wa Mbuji-Mayi, waandishi hao wa habari walikuwa wakiongozana na wajumbe wa mashirika yasiyo yakiserikali watu kadhaa waliokuja kuonyesha mshikamano wao.

Hadi Alhamisi hii mchana, hakuna radio au runinga katika mji wa Mbuji-Mayi, ambayo ilisikika ikirusha matangazo yake. RTNC imeanza kurusha matangazo yake kuanzia saa siata mchana saa za DR Congo. Wakati huo huo, uchunguzi kuhusu mauaji hayo unaendelea. Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Kasai-Mashariki, Ngoyi Kasanji, "watu wanaoshukiwa kuhusika katika mauaji hayowamekamatwa" na "sheria itafuata mkondo wake."

Marcel Lubala aliuawa akiwa nyumbani kwake na watu wenye silaha ambao kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la 'Journaliste en Danger' , watu waliokua wamevaa "sare za kijeshi" walimuua mwandishi wa habari Marcel Lubala kwa kumpiga "risasi tatu shingoni na tumboni." Kwa mujibu wa shirika hilo, Marcel Lubala aliitwa na Idara ya Ujasusi ya DR Congo (ANR) siku moja kabla ya kifo chake ili kutoa mwanga kuhusu "kesi ya familia".

Marcel Lubala ni mwandishi wa habari wa kumi na nne kuuawa katika mazingira ya kikazi ndani ya kipindi cha miaka kumi nchini DR Congo.