DRC-UNESCO

UNESCO yaitaka DRC kuwafungulia mashtaka wauaji wa mwanahabari Marcel Lubala

Irina Bokova, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO
Irina Bokova, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO KENA BETANCUR / AFP

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Irina Bokova, anaitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhakikisha kuwa wale wote waliotekeleza mauaji ya mwanahabari wa Televisheni na Redio ya taifa Marcel Lubala wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Lubala aliuawa na watu wasiofahamika wiki iliyopita akiwa nyumbani kwake mjini Mbuji-Mayi.

Mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 59, alikuwa mfanyikazi wa kituo hicho cha taifa RTNC kwa muda wa miaka 15.

“Nalaani mauaji ya Marcel Lubala. Wanahabari wanastahili kufanya kazi zao za kuwajuza wananchi bila ya kuogopa lolote,” amesema Bokova.

“Naamini kuwa serikali ya DRC itafanya uchunguzi huru na wale wote waliohusika watafunguliwa mashataka,” ameongeza Bokova.

Viongozi wa mkoa wa Kasai-Oriental, wanasema tayari uchunguzi umeshaanza kubaini hasa ni akina nani waliotekeleza mauaji hayo.

Joseph Tshilunde, rais wa muungano wa waandishi wa Habari nchini DRC (UNPC), amesema kwa kipindi cha miaka 10 zilizopita, wanahabari 16 wameuawa nchini humo katika mazingira ya kutatanisha.

Shirika la Kimataifa la wanahabari wasiokuwa na mipaka (RSF), linaiorodhesha DRC katika nafasi ya 152 kati ya mataifa 180 mwaka 2016 kueleza namna mataifa mbalimbali yanavyoheshimu haki za wanahabari duniani.