SENEGAL-UHALIFU

Macky Sall: tutaongeza adhabu

Rais wa Senegal Macky Sall alaani visa vya mauaji ambavyo vimekithiri katika baadhi ya maeneo nchini mwake..
Rais wa Senegal Macky Sall alaani visa vya mauaji ambavyo vimekithiri katika baadhi ya maeneo nchini mwake.. Source : mycitypapers.com

Rais wa Senegal ametangaza mageuzi ya sera ya adhabu kwa ajili ya kuwahukumu maisha jela wahusika katika mauaji nchini Senegal.

Matangazo ya kibiashara

Katika maneno yaliyorushwa na vyombo vya habari nchini Senegal na kunukuliwa na shirika la habari la AFP, Rais Macky Sall amehakikisha kwamba mabadiliko haya yatajadiliwa katika kikao cha baraza la mawaziri kiliopangwa kufanyika Alhamisi wiuki hii.

"Tutaongeza adhabu na kuhakikisha kwamba mtu yeyote atakayefupisha maisha ya binadamu atatumikia kifungo cha maisha jela, bila kupewa na nafasi ya kuepuka hatua hii," amesema Macky Sall.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Senegal, Macky Sall ametangaza hatua hii wakati wa mazishi ya Naibu Mwenyekiti wa baraza la Uchumi, Jamii na Mazingira (Cese), Fatoumata Mactar Ndiaye, aliyechinjwa nyumbani kwake Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita katika kitongoji cha Pikine, mjini Dakar.

Bw. Sall pia ameelezea mauaji yaliyotokea Oktoba 27 ya dereva wa teksi ambaye alipigwa risasi na kuuawa na dereva mwengine baada ya mabishano katika kituo cha mafuta mjini Dakar.

Muuaji wa Fatoumata Mactar Ndiaye, dereva wake, aliyekamatwa muda mfupi baadaye, alikiri kufanya kitendo hicho kiovu, alisema Jumapili mwendesha mashitaka, Serigne Bassirou Gueye.