MISRI

Mahakama yamwondolea Morsi adhabu ya maisha jela

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi akiwa kizimbani
Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi akiwa kizimbani DR

Mahakama ya juu ya rufaa nchini Misri imeondoa adhabu ya maisha jela, aliyokuwa amepewa rais wa zamani wa nchi hiyo Mohammed Morsi.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama hiyo sasa inataka Morsi mwenye umri wa miaka 65 afunguliwe mashtaka upya.

Kabla ya uamuzi huo wa awali, alikuwa ameshtakiwa kwa kushirikiana na makundi ya kigaidi kutoka nje ya nchi kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Hatua hii ya leo imekuja wiki moja baada ya Mahakama pia ya rufaa kuamuru kuwa Morsi ashtakiwe upya kwa madai ya kuchochea kuvunjwa kwa gereza mwaka 2011.

Kutokana na kosa hilo, Mahakama ilikuwa imempa adhabu ya kifo lakini adhabu hiyo imeondolewa.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa zamani aliyemwondoa madarakani Hosni Mubarak mwaka 2011, bado anakabiliwa na vifungo vingine viwili katika kesi mbili tofauti.

Morsi alikuwa kiongozi wa kundi la Muslim Brotherhood ambalo kwa sasa limefungiwa kwa madai kuwa ni la kigaidi, alichaguliwa rais mwaka 2012 lakini akaondolewa madarakani mwaka mmoja baadaye baada ya maandamano ya umma dhidi ya ungozi wake.