DRC-MAREKANI

Marekani yaukosoa upinzani nchini DRC kuhusu hali ya kisiasa

Etienne Tshisekedi, kiongozi wa upinzani nchini DRC alipowasili nchini Julai 21 2016 jijini Kinshasa katika mkutano wa upinzani
Etienne Tshisekedi, kiongozi wa upinzani nchini DRC alipowasili nchini Julai 21 2016 jijini Kinshasa katika mkutano wa upinzani RFI/Sonia Rolley

Marekani inawataka wanasiasa wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuacha kutoa matamshi yanayoweza kuchochea zaidi hali ya kisiasa nchini humo baada ya mwafaka wa kisiasa kupatikana hivi karibuni.

Matangazo ya kibiashara

Ubalozi wa Marekani jijini Kinshasa umemtaka kiongozi wa kundi la upinzani Rassemblement  Étienne Tshisekedi, kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha hali ya kidemokrasia nchini humo.

“Tunawaomba wapinzani wa Rassemblement wanaoongozwa na Ettiene Tshisekedi waache kutoa maneno yanayoweza kurudisha nyuma hali ya kidemokrasia lakini waje na mapendekezo ya kusaidia hali hii ,” taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani jijini Kinshasa imeeleza.

Kauli hii imekuja wakati huu upinzani ukiendelea kukataa kutambua mwafaka wa kisiasa uliofikiwa mwezi Oktoba mwaka huu kati ya serikali na baadhi ya wanasiasa wa upinzani, kutaka kuwepo kwa serikali ya mpito kwa muda wa miaka miwili na baadaye uchaguzi wa urais kufanyika mwaka 2018.

Kutekeleza makubaliano haya, wiki iliyopita rais Joseph Kabila alimteua Samy Badibanga mwanasiasa wa upinzani na mshirika wa zamani wa Tshisekedi kuhudumu katika nafasi ya Uwaziri Mkuu.

Uteuzi huu unapingwa na wanasiasa hao wa Rassemblement ambao pia wanadai Badibanga ni raia pia wa Ubelgiji na hivyo hawezi kuwa Waziri Mkuu kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Rais Kabila amewaomba Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo kusaidia kupata mwafaka kati ya wanasiasa waliotia saini mkataba huo na wale wa Rassemblement ili kufanikisha serikali hiyo ya mpito lakini wanasiasa hao wa upinzani wanaendelea kushinikiza kuwa ni lazima rais Kabila aachie madaraka ifikapo mwezi Desemba mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Serikali ya DRC imekuwa ikisema miundombinu kama fedha za kuandaa uchaguzi huo, kutowepo kwa daftari la wapiga kura na ukosefu wa hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo, hairuhusu uchaguzi kufanyika mwaka huu.