`ZIMBABWE

Harare: Mahakama ya ahirisha kesi ya wanajeshi wa zamani kwa muda usiojuliakana

Mahakama nchini Zimbabwe, juma hili imeahirisha kwa muda usiojulikana, kesi ya maveterani wa tano waliopigana vita vya ukombozi nchini humo, ambapo walishtakiwa kwa kosa la kumkashifu Rais Robert Mugabe, mahakama ikisema mwendesha mashtaka hana kesi.

Rais wa Zimbabawe, Comrade Robert Mugabe, ambaye sasa yuko kwenye shinikizo la kutakiwa kujiuzulu.
Rais wa Zimbabawe, Comrade Robert Mugabe, ambaye sasa yuko kwenye shinikizo la kutakiwa kujiuzulu. REUTERS/Philimon Bulawayo
Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi hao wa tano wa zamani, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutoa matamshi ya uchochezi, wakimtuhumu Rais Mugabe kuwa ana tabia za "Kidikteta" na walikamatwa mapema mwaka huu katika msako ulioendeshwa dhidi ya wakosoaji wa utawala wa Rais Mugabe.

Hata hakimu mkazi wa mahakama ya Harare, Mujuya Chastised, amekosoa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali kushindwa kuanza kesi hiyo kwa wakati ambapo alikataa ombi jingine la kuahirisha kesi hiyo kwa siku moja zaidi.

"Ninakataa ombi la kuongeza muda zaidi wa watuhumiwa kubaki rumande," alisema hakimu Mujuya. Ambapo akaongeza "Utata wenu endeleeni kukaa nao huko huko ofisini kwenu."

Watano hao, sasa watashuhudia dhamana zao zikirejeshwa.

Ili kesi hiyo ianze upya, upande wa mwendesha mashta utalazimika kuwasilisha jala jipya la kesi hiyo na kutuma notisi kwa baraza la kitaifa la wanajeshi wakongwe waliopigana vita vya ukombozi nchini humo, kuwataarifu nia yao ya kufungua upya kesi hiyo.

Katika taarifa yao, wapiganaji hao wa zamani kwenye miaka ya 1970, awali walikuwa wakimuunga mkono Rais Mugabe, lakini baadae wakawa wakosoaji wakubwa wa utawala wake na kudai kuwa hawatamuunga mkono ikiwa atawania tena kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Tayari chama tawala nchini Zimbabwe cha Zanu- PF, kimeshamteua Rais Mugabe kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2018.

Rais Mugabe, amekuwa madarakani toka mwaka 1980, anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka ndani ya chama chake na nje ya nchi yake, akishinikizwa kujiuzulu kutokana na kuendelea kuzorota kwa uchumi wa taifa hilo.