GAMBIA

Rais Jammeh asema maandamano hayataruhusiwa baada ya Uchaguzi

Rais wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa Gambia Yahya Jammeh Reuters/Lucas Jackson

Raia wa Gambia watapiga kura kesho kumchagua rais.

Matangazo ya kibiashara

Rais Yahya Jammeh ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo kwa miaka 22 sasa, anawania tena wadhifa huo akikabiliwa na mpinzani mmoja, Adama Barrow.

Akimalizia kampeni yake siku ya Jumanne jijini Banjul, kiongozi huyo alisema hakuna maandamano yoyote yatakayokubaliwa baada ya uchaguzi huo.

Aidha, amewaambia wananchi wa taifa lake kuwa hawatawahi kumpata kiongozi kama yeye na kuonya kuwa yeyote atakayezua fujo baada ya uchaguzi kukamilika, atachukuliwa hatua kali.

“Sisemi kuwa mimi ndio bora, lakini ukweli wa mambo ni kwamba hamtawahi kumpata kiongozi kama mimi,” alisema Jammeh.

“Nawaomba mwende mkapige kura na mfanye maamuzi ya dhati mkiheshimu Mwenyezi Mungu na nia zenu za ndani,”.

Naye mgombea pekee wa upinzani katika uchaguzi huu ameimbia RFI kuwa ana uhakika wa kushinda uchaguzi huu na kuleta mabadiliko ya kweli nchini humo.

“Nina unahakika nitashinda na kuleta ushindi kwa upinzani,” alisema Barrow.

“Sina uhakika hata hivyo ikiwa zoezi hilo litakuwa huru na haki lakini acha tuone,”.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya na wanahabari wa Kimataifa wamenyimwa vibali kwenda kushuhudia uchaguzi huo.

Wachambuzi wa siasa nchini Gambia wanasema kuwa rais Jammeh anatarajiwa kuchaguliwa tena katika taifa hilo.