GAMBIA

Rais Jammeh anakabiliwa na ushindani mkubwa uchaguzi wa Gambia

Raia wa Gambia wanapopiga kura kumchagua rais atakayehudumu kwa muda wa miaka mitano ijayo, rais Yahya Jammeh ambaye ameongoza nchi hiyo kwa miaka 22 , kwa mara ya kwanza anakabiliwa na ushindani mkali.

Makao makuu ya Tume ya Uchaguzi nchini Gambia  Serekunda jijini Banjul kwa maandalizi ya kupiga kura
Makao makuu ya Tume ya Uchaguzi nchini Gambia Serekunda jijini Banjul kwa maandalizi ya kupiga kura REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Ushindani huo unatoka kwa mgombea wa upinzani mfanyibiashara Adama Barrow, anayewakilisha muungano wa vyama saba vya upinzani katika Uchaguzi huu.

Wapiga kura wapatao 880,000 wanapiga kura katika vituo 1400 kuamua kiongozi wao.

Rais Jammeh anawania urais kwa muhula wa tano sasa chini ya chama tawala cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC) na kusema hakuna rais bora ambaye raia wa nchi hiyo wanaweza kumpata kama yeye.

Wadadisi wa siasa nchini humo wanasema kuwa hatua ya vyama vya upinzani kuungana ili kupambana na rais Jammeh ni ishara kuwa mambo hayatakuwa mepesi kipindi hiki.

Hata hivyo, rais Jammeh ameonya kuwa hakuna atakayeruhusiwa kuandamana baada ya matokeo ya mwisho kutolewa kwa kile alichokieleza kuwa kura haziwezi kuibiwa kutokana na mfumo wa kipekee unaotumiwa kupiga kura nchini humo.

Mgombea mwingine wa upinzani Mama Kandeh, anawania pia urais kupitia chama cha Gambian Democratic Congress (GDC).