GAMBIA

Mfahamu rais mpya wa Gambia

Rais mpya wa Gambia  Adama Barrow hapa alikuwa ni wakati wa kampeni
Rais mpya wa Gambia Adama Barrow hapa alikuwa ni wakati wa kampeni REUTERS/Thierry Gouegnon

Gambia imempata rais mpya atakayeongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka mitano ijayo kuchukua nafasi ya rais Yahya Jammeh.Lakini Adama Barrow ni nani ?

Matangazo ya kibiashara

Barrow ni mwanasiasa na Mfanyibiashara nchini Gambia mwenye umri wa miaka 51.

Mwaka 2000 alikwenda jijini London nchini Uingereza alikofanya kazi kama mlinzi katika kampuni mmoja huku akimalizia masomo yake ya maswala ya Biashara.

Mwaka 2006, alirejea nyumbani na kuanzisha kampuni yake ya ujenzi na kuanza kujihusisha na maswala ya siasa.

Mwaka huu, vyama saba vya upinzani viliungana na kumteua kuwa mgombea wake wa  urais kupambana na rais Yahya Jammeh ambaye ameongoza nchi hii kwa muda wa miaka 22.

Kipindi chote cha kampeni, Barrow alishtumu kutokuwepo kwa mihula ya uongozi nchini humo na kushtumu hatua ya uongozi wa Jammeh kuwafunga wanasiasa wa upinzani.

Barrow aliahidi kuunda serikali ya mpito kwa muda wa miaka mitatu itakayojumuisha wanasiasa kutoka vyama vyote vya upinzani vilivyounda muungano huo.

Ushindi wake umeleta furaha kubwa nchini humo, huku raia wengi wakisema ni ushindi wa kuikomboa nchi hiyo baada ya miaka 22 ya uongozi wa rais Jammeh.

Adama Barrow sasa ana kazi ya kuleta mwamko mpya katika taifa hilo la Afrika Magharibi kwa miaka mitano ijayo.