BURUNDI-USALAMA

Maafisa wa Jeshi Burundi wakamatwa kufuatia shambulizi dhidi ya Nyamitwe

Willy Nyamitwe alishambuliwa kwa risasi Jumatatu usiku juma lililopita na watu ambao hawajajulikana, huku mmoja wa walinzi wake na dereva wakiuawa.
Willy Nyamitwe alishambuliwa kwa risasi Jumatatu usiku juma lililopita na watu ambao hawajajulikana, huku mmoja wa walinzi wake na dereva wakiuawa. © Getty Images

Maafisa watatu wa jeshi la burundi wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la kumuua mshauri wa raisi wa Burundi,Willy Nyamitwe kwa mujibu wa polisi na vyanzo vya kiusalama.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio hilo lilitekelezwa jumatatu baada ya kundi la watu waliojihami kwa silaha kumshambulia Willy Nyamitwe msemaji wa serikali alipokuwa akirejea nyumbani kwake jijini Bujumbura.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi mjini Bujumbura Pierre Nkurikiye shambulio hilo ni ugaidi,kama alivyochapisha katika ukurasa wake wa twita.

Imeelezwa kuwa makanali wawili na kaptaini mmoja walitiwa nguvuni kufuatia jaribio la mauaji ambayo mmoja wa walinzi wa Willy Nyamitwe na dereva waliuawa.

Umoja wa ulaya ulilaani shambulio hilo na kukumbusha kwamba "ufumbuzi wa kisiasa kwa njia ya mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote ndio njia sahihi ya kupelekea nchi hiyo kuondokana na mgogoro huo, na hali hiyo ndio itakayo rejesha amani na usalama nchini Burundi ".