MALAWI

Maandamano makubwa yafanyika nchini Malawi kupinga utoaji mimba na ushoga

Wanaume wawili wakionekana katika picha wakibusiana, jijini Rio Brazil
Wanaume wawili wakionekana katika picha wakibusiana, jijini Rio Brazil REUTERS/Bruno Domingos/File Photo

Maelfu ya waandamanaji, wengi wakiwa ni waumini wa dini ya Kikristo, wameandamana kwenye miji mbalimbali nchini Malawi, wakipinga mapendekezo ya kuhalalisha vitendo vya utoaji mimba na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsi moja.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano haya ya amani, yaliandaliwa na kanisa Katoliki kwa kushirikiana na yale makanisa ya Kiinjili nchini Malawi, ambako suala la ngono na mapenzi ya jinsia moja ni masuala yasiyotamkwa hadharani.

Waandamanaji wanaokadiriwa kufikia elfu 2 waliandamana jijini Blantyre, huku zaidi ya elfu 1 wakiandamana jijini Lilongwe yaliko makao makuu ya Serikali.

Waandaaji waliwasilisha maombi yao Serikalini wakikashifu vitendo vya utoaji mimba na kuhalalishwa kwa mapenzi ya jinsi moja.

Rasimu iliyowasilishwa bungeni ambayo inaruhusu utoaji mimba, ambapo chini ya sheria hii inaruhusu tu pale mtu anapobakwa au mama anapokuwa hatarini kupoteza maisha.

Nchi ya Malawi, pia imepanga kufanya mjadala wa uma kuamua ikiwa kufanyike mabadiliko ya sheria ambazo zinakataza vitendo vya ushoga na usagaji nchini humo.

"Utoaji mimba na ushoga ni mambo ya kishetani na dhambi kubwa. Tunataka tusimamie kupinga utamaduni wa kuunga mkono vifo na tisho kwa maisha ya binadamu," alisema padri Francis Tambala wakati akiwahutubia waandamanaji jijini Blantyre.