ICC-UGANDA

Majaji wa mahakama ya ICC waanza kusikiliza namna Ongwen alivyotekeleza ubakaji

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC ICC court Room1 Screenshot

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, wameanza kusikiliza maelezo ya awali ya upande wa waendesha mashtaka katika kesi dhidi ya aliyekuwa kamanda wa kundi la waasi wa Uganda, LRA, Dominic Ongwen.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya Jumanne ya wiki hii kusomewa mashtaka 70, yakiwemo makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, Jumatano ya Desemba 7 majaji wa mahakama ya ICC wameanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Juma hili akiulizwa ikiwa alihusika katika uhalifu wowote ndani ya kundi la LRA, Dominic Ongwen alikana mashtaka dhidi yake na kusisitiza kuwa muhisika mkuu ni Joseph Kony, kiongozi wa kundi hilo.

Waendesha mashtaka wameelezea namna ambavyo Dominic Ongwen akiwa kama kamanda wa operesheni za uvamizi wa kundi la LRA, alishiriki kuvamia makambi ya raia na vijiji, ambako wapiganaji wake waliwateka vijana wadogo na wasichana ambao baadae waliishia kuwa wake zao.

Waendesha mashtaka wameeleza kuwa, Ongweni akiwa na walinzi wake, walivamia moja ya kijiji kilichoko kaskazini mwa Uganda, ambako waliwateka wasichana wadogo na baadae waliwalazimisha kuwafanyia kazi za ndani na kuwageuza wake zao.

"Ongweni alimchukua shahidi namna 0099 na kumfanya mjakazi wake na kisha baadae kumlazimisha kufanya nae ngono, kitendo ambacho Ongwen alikifanya kwa kulazimisha, alimbaka shahidi huyo mara moja, mara mbili na kisha tena na tena hadi aliporidhika na baadae kuanza kucheka sambamba na wapiganaji wengine". walisema waendesha mashtaka.

Waendesha mashtaka wameendelea kuwaeleza majaji wa mahakama hiyo mwaka hadi mwaka namna ambavyo wapiganaji wa LRA na hasa waliokuwa chini ya Ongwen, waliwateka wasichana na kuwalazimisha kufanya nao ngono na kuwafanya watumwa wa ngono, na kwa waliokataa waliishia kuuawa.