MISRI-USALAMA

Sisi: muhusika mkuu wa shambulizi baya dhidi ya kanisa la Coptic ajulikana

Mazishi ya wahanga wa mashambulizi katika kanisa la Coptic yafanyika mjini Cairo Jumatatu 12 Desemba.
Mazishi ya wahanga wa mashambulizi katika kanisa la Coptic yafanyika mjini Cairo Jumatatu 12 Desemba. Khaled DESOUKI / AFP

Jumatatu hii Desemba 12 waumini wa kanisa la Coptic nchini Misri wamefanya sherehe ya mazishi ya watu 24 waliouawa siku moja kabla katika shambulio la bomu lililoendeshwa katika kanisa la Mtakatifu Petro na Mtakatifu Paulo katika mji wa Cairo, waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP walishuhudia.

Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya waumini wa kanisa hilo walikusanyika katika kanisa la Bikira Maria, ambapo majeneza ya waathirika yalikua yamewekwa karibu na madhabahu.

Akizungumza, Papa Tawadros II, kiongozi wa kanisa la Coptic, amelitaja shambulizi hilo kama "shambulizi dhidi ya Wamisri." "Tunasikitishwa sana" kwa vifo vya waumini ", lakini pia kwa mabaya yote haya yanayoendeshwa dhidi ya binadamu," Papa Tawadros II amesema, huku akitokwa na machozi.

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi hilo imeongezeka na kufikia Jumatatu hii hadi 24, imesema wizara ya afya ya Misri , ambayo awali ilitaja idadi ya watu 23 kuwa ndio waliuawa katika shambulizi hilo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya, watu 24 waliokua wamejeruhiwa waliondoka hospitali Jumatatu hii asubuhi na 21 bado wanalazwa hospitalini. Waathirika wengi ni wanawake.

Mshambuliaji wa kanisa la Coptic ajulikana

"Mshambuliaji ni Mahmoud Mostafa Mohamed Shafiq, mwenye umri wa miaka 22 na alijilipua kwa kutumia mkanda wenye vilipuzi, haikuwa bomu," amesema rais Sissi. Ameongeza kuwa watu wanne waliohusika katika shambulizi hilo, wanaume watatu na mwanamke mmoja, wamekamatwa na wengine bado wanatafutwa.

Mlipuko ulitokea Jumapili saa 4:00 mchana saa za Misri (sawa na 2:00 asubuhi saa za kimataifa) ndani ya kanisa, karibu na kanisa Kuu la Coptic la Mtakatifu Mark, makao makuu ya Papa Tawadros II.