DRC-KABILA-VATICA

Mzozo wa Kisiasa DRC: Mazungumzo ya lala salama kabla ya Desemba 19

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis wakati alipokutana na rais wa DRC, Joseph Kabila, Septemba 26, 2016 mjini Vatican, maaskofu wa kanisa lake wanasimamia mazungumzo ya kusaka muafaka
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis wakati alipokutana na rais wa DRC, Joseph Kabila, Septemba 26, 2016 mjini Vatican, maaskofu wa kanisa lake wanasimamia mazungumzo ya kusaka muafaka REUTERS/Andrew Medichini/Pool

Mazungumzo ya kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, kabla ya kumalizika kwa muhula wa rais Joseph Kabila, yameendelea Jumamosi hii, lakini wapatanishi wanao muda mfupi sana kufikia makubaliano. 

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo haya yanaonekana kama ndio juhudi za mwisho kabla ya Desemba 19 mwaka huu, ambapo ndio utakuwa muda wa mwisho wa rais Joseph Kabila kuwa madarakani kwa mujibu wa katiba, lakini hata hivyo amedhamiria kusalia madarakani baada ya makubaliano ya miezi michache iliyopita na kusogezwa mbele kwa uchaguzi.

Wadau, wawakilishi na wafuasi wa chama tawala, upinzani na baraza la maaskofu wa kanisa katoliki, CENCO, ambao ndio wapatanishi wakuu, wamekutana kuanzia saa tano Asubuhi Desemba 17.

Mazungumzo haya yalianzishwa Desemba 8 na baraza la maaskofu wa kanisa katoliki, yalikuwa yamalizike Ijumaa ya Desemba 16, lakini yalilazimika kusogezwa mbele kwa siku moja zaidi baada kukosekana kwa makubaliano na muungano mkuu wa upinzani.

Wajumbe wa baraza la maaskofu wanatarajiwa kusafiri kwenda Vatican jioni ya Jumamosi ya Desemba 17 na kurejea Jumanne ya Desemba 20, terehe ambayo rais mpya anatakiwa kula kiapo.

Mazungumzo haya yanalengo la kutafuta muafaka kuhusu uundwaji wa Serikali ya mpito, itakayopelekea kufanyika kwa uchaguzi mkuu kupata mrithi wa rais Joseph Kabila aliyeko madarakani toka mwaka 2001 na katiba haimruhusu kuendelea kuwa madarakani wala kuwania tena kiti hicho.

Kinara wa upinzani aliyetia saini makubaliano ya awali, Vital Kamerhe, ameonesha matumaini ya kufikiwa makubaliano.