DRC-SIASA

Tshisekedi ataka kutotambuliwa kwa rais Kabila huku Badibanga akiunda serikali

Kiongozi wa upinzani nchini DRC  Etienne Tshisekedi
Kiongozi wa upinzani nchini DRC Etienne Tshisekedi Yutube

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini DRC Etienne Tshisekedi amewataka raia wa nchi hiyo kutomtambua rais Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo baada ya muda wake wa kikatiba kumalizika.

Matangazo ya kibiashara

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 84, akizungumza kupitia mkanda wa video, amewataka wafuasi wa upinzani kujitokeza na kuandamana kwa amani kumpinga rais Kabila lakini pia mataifa ya kigeni kutomtambua.

Muda mfupi baada ya muhula wa rais Kabila kukamilika kikatiba, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito Samy Badibanga alitangaza Baraza lake la Mawaziri.

Waziri Mkuu Samy Badibanga
Waziri Mkuu Samy Badibanga JUNIOR D.KANNAH / AFP

Baadhi ya Mawaziri wa serikali ya mpito:

  • Waziri Mkuu:- Samy Badibanga
  • Naibu Waziri Mkuu/ Waziri wa Mambo ya nje:- Leonard She Okitundu
  • Naibu Waziri Mkuu/ Waziri wa Mambo ya ndani:-  Emmanuel Ramazani Shadary
  • Naibu Waziri Mkuu/ Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano:- José Makila
  • Waziri wa Sheria na Katiba:- Alexis Thambwe-Mwamba
  • Waziri wa Mawasiliano:- Lambert Mende

Kuundwa kwa serikali ya mpito kulikuja baada ya mazungumzo ya amani yaliyoongozwa na msuluhishi wa Umoja wa Afrika Edem Kodjo, lakini yakasusiwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani vinavyounda muungano wa Rassemblement chini ya uongozi wa Etienne Tshisekedi wa chama cha UDPS.

Wanasiasa wa UDPS wamelaani kuundwa kwa serikali hii huku mazungumzo mapya yakiendelea na yanatarajiwa kurejelewa siku ya Jumatano.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaona kuwa huenda mazungumzo hayo yanayoongozwa na Kanisa Katoliki, yasizae matunda kwa sababu ya kuundwa kwa serikali hii lakini pia Tshisekedi kutaka maandamano ya kumshinikiza rais Kabila kuondoka madarakani.