UNHCR-SUDAN

Wafanyakazi watatu wa UNHCR waliotekwa Darfur waachiliwa huru

Umoja wa Mataifa unasema wafanyakazi watatu wa Shirika la wakimbizi UNHCR waliokuwa wametekwa nyara mwezi uliopita katika jimbo la Darfur, wameachiliwa huru.

Askari wa UNAMID akipiga doria katika jimbo la Darfur tarehe 12 Januari mwaka 2015.
Askari wa UNAMID akipiga doria katika jimbo la Darfur tarehe 12 Januari mwaka 2015. ASHRAF SHAZLY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wafanyakazi hao watatu Sarun Pradhan na Ramesh Karki kutoka Nepal na Musa Omer Musa Mohamed wa Sudan, walitekwa tarehe 27 mwezi Novemba katika eneo la El Geneina Magharibi mwa jimbo la Darfur.
Umoja wa Mataifa umeishukuru serikali ya Khartoum kwa kusaidia kuachiliwa huru kwa wafanyakazi hao na kueleza kuwa, hii itasaidia kuendeleza kazi inayofanywa na Shirika hilo.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa haujaeleza ni vipi wafanyakazi hao waliachiliwa huru na vipi serikali ya Sudan ilivyosaidia.

Hii sio mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa Shirika la UNHCR kutekwa katika jimbo la Darfur katika miaka ya hivi karibuni.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukituma misaada ya kibinadamu na kuwasaidia maelfu ya watu ambao wameyakimbia makazi yao baada ya machafuko yaliyosababisha zaidi ya watu laki tatu kupoteza maisha katika mapigano yaliyoanza mwaka 2003.