DRC - SIASA

Hatuwa chanya yafikiwa kuelekea makubaliano nchini DRCongo

wanasiasa wa DRCongo, Samy Badibanga, Vital Kamerhe
wanasiasa wa DRCongo, Samy Badibanga, Vital Kamerhe JUNIOR D.KANNAH / AFP

Utulivu umerejea katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo Kinshasa, huku hofu ikiendelea kuripotiwa katika miji mingine ya nchi hiyo, viongozi wa serikali wanasema watu 22 ndio waliopoteza maisha, lakini mashirika ya kiraia yanasema ni watu 34. Huenda wanasiasa wa upinzani na Utawala wakafikia makubaliano hii leo Ijumaa, baada ya kukubaliana mambo muhimu.

Matangazo ya kibiashara

Waziri mkuu mpya wa nchi hiyo Samy Badibanga amekula kiapo hapo jana kuiongoza serikali mpya ya nchi hiyo na ambapo amesisitiza kuhusu swala la uheshimishwaji wa haki za binadamu, huku akiweka wazi yale yatayopewa kipao mbele katika serikali yake.

Baraza la Maaskofu wa kanisa katoliki nchini humo CENCO linaendelea kuwashinikiza wanasiasa kuhakikisha muafaka unapatikana baina ya wawakilishi 16 wa Utawala na upinzani.

Mazungumzo hayo yamepiga hatuwa chanya licha ya pande hizo mbili kutofautiana katika baadhi ya mambo, kuna asilimia kubwa ya kufikiwa muafaka hii leo na pande zote 2 kusaini makubaliano.

Joto la kisiasa limepamba moto nchini DRCongo tangu pale ulipotamatika muhula wa rais Joseph Kabila bila kupatikana mrithi wake. Kanisa Katoliki nchini humo limewataka wanasiasa kuhakikisha wamekubaliano kabla ya siku kuu za chrismas kuliepusha taifa hilo kutumbukia katika lindi la machafuko.

Miongoni mwa yale ambayo pande hizo zimekubaliana, ni pamoja na uchaguzi kufanyika mwisho wa mwaka 2017 badala ya April 2018 kama ilivyokuwa imekubaliwa hapo awali.

Baraza la mawaziri wa serikali ya muungano wa kitaifa litaundwa, waziri mkuu atatoka upande wa upinzani, lakini haifahamiki iwapo Samy Badibanga aliekula kiapo jana alhamisi atasalia kwenye nafasi hiyo.

Serikali ya mpito itaongozwa na rais Joseph Kabila hadi uchaguzi utapofanyika, lakini anatakiwa kuweka bayana kwamba hatobadili katiba kwa ajili ya kuwania uchaguzi, na tume ya kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano itaundwa, huku maaskofu wakipendekezwa kuongoza tume hiyo, wakati huo huo maaskofu wakipendekeza kuihusisha pia Jumuiya ya Kimataifa.

katika hatuwa nyingine, watu 11 wampoteza maisha katika kijiji cha Manono jimbo la Katanga, wakati wa mapigano baina ya watu wa kabila la Mbilikimo na waluba huku watu wengine 94 wakijeruhiwa.