CONGO-MAREKANI

Ziara ya Dennis Sassou-Ngueso yazua utata nchini Marekani

Rais Denis Sassou-Nguesso yuko mamlakani kwa kipindi cha miaka 32 nchini Congo-Brazzaville.
Rais Denis Sassou-Nguesso yuko mamlakani kwa kipindi cha miaka 32 nchini Congo-Brazzaville. © Wikimedia

Utata umezuka katika ziara ya Rais wa Congo-Brazaville Denis Sassou-Nguesso nchini Marekani kukutana na rais mteule Donald Trump.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema kuwa watu wa karibu wa Trump hawafahamu kuhusu ziara hiyo na mpango wa kukutana na rais huyo mteule anayetarajiwa kuapishwa wiki ijayo.

Akinukuliwa na shirika la habari la Reuters, msemaji wa Donald Trump amesema kuwa rais mteule wa Marekani hajapanga kukutana na mwenzake wa Congo-Brazaville.

Hata hivyo, Msemaji wa serikali ya Congo na Waziri Mawasiliano Thierry Moungalla ametangaza katika taarifa rasmi iliyosainiwa na ofisi ya rais kuwa viongozi hao watakutana jimboni Hawai nchini Marekani.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa rais Nguesso angepokelewa kama mwenyekiti wa Kamati maalum ya Umoja wa Afrika AU kuhusu maswala ya Libya ili kutafuta njia za kupata suluhu ya mgogoro wa nchi hiyo pamoja na masuala ya kimataifa barani Afrika.

Watu wa karibu wa Trump wanasema hakuna mkutano wowote kama huo.