DRC-SIASA-KABILA

DRC: Mazungumzo kuhusu utekelezaji wa makubaliano kuanza juma hili

Pande zinazokinzana katika mzozo wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, juma hili zinatarajiwa kuwa na mazungumzo ya kwanza kuhusu kuanza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwishoni mwa juma lililopita, wapatanishi wamesema.

Askofu Marcel Utembi, rais wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC, ambao wamesimamia kufikiwa kwa makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa juma.
Askofu Marcel Utembi, rais wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC, ambao wamesimamia kufikiwa kwa makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa juma. REUTERS/Robert Carrubba
Matangazo ya kibiashara

"Mkutano wa awali kuamua kuhusu njia zitakazotumiwa kutekeleza makubaliano, umepangwa kufanyika Jumanne," amesema msemaji wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC, Father Donatien Nshole.

Makubaliano yaliyofikiwa baada ya majadiliano makali ya usiku wa kuamkia mwaka mpya, yanalenga kumaliza sintofahamu ya kisiasa nchini humo kuhusu mustakabali wa rais Joseph Kabila.

Kwa mujibu wa katiba ya DRC, raia Kabila mwenye umri wa miaka 45 hivi sasa, alitakiwa kuwa ameondoka ofisini Desemba 20 ambao ndio ulikuwa mwisho wa muhula wake wa pili na wa mwisho, lakini hakuonesha nia ya kuondoka wakati huu.

Kwa mujibu wa makubaliano haya, rais Kabila ataendelea kusalia madarakani hadi pale uchaguzi mkuu mpya utakapofanyika "mwishoni mwa mwaka 2017."

Masuala muhimu yanayitarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huu muhimu, ni pamoja na njia itakayotumika kuwachagua wajumbe 20 wa baraza la mpito, CNSAP, pamoja na uundwaji wa Serikali ya mpito.

Kwa upande wa Serikali, waziri wa mawasiliano, Lambert Mende, amesema mazungumzo haya yatapaswa kupata suluhu ya tatizo lililopo hasa la "utangamano", akitolea mfano kuhusu suala la vyama vingine 10 ambavyo vinaiunga mkono Serikali na havijatia saini makubaliano haya.

Vyama hivyo 10, pia kimo chama cha Congo Liberation Movement (MLC) cha aliyewahi kuwa makamu wa rais Jean-Pierre Bemba, ambaye hivi sasa anatumikia kifungo kwenye gereza la Uholanzi baada ya kupatikana na hatia katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

MLC kinasema kutotia kwake saini makubaliano hayo, kusitumiwe na baadhi ya wanasiasa kama njia ya kushindwa kutekeleza makubaliano ya mwishoni mwa juma.