GAMBIA

Mkuu wa tume ya Uchaguzi Gambia akimbilia Senegal

Mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Gambia, amekimbia nchi yake na kukimbilia nchini Senegal, akihofia njama zilizopangwa dhidi yake mwezi mmoja tu baada ya kutangaza rais Yahya Jammeh ameshindwa katika uchaguzi na kumaliza utawala wake wa miaka 22, familia yake imesema.

Kwa mujibu wa Alieu Momar Njai, Adama Barrow (pichani) ni mshindi wa uchaguzi wa rais, hapa ilikua Novemba 29, 2016.
Kwa mujibu wa Alieu Momar Njai, Adama Barrow (pichani) ni mshindi wa uchaguzi wa rais, hapa ilikua Novemba 29, 2016. REUTERS/Thierry Gouegnon
Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa ndugu zake ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa "mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi, Alieu Momar Njie, amekimbilia nchini Senegal baada ya kupata taarifa kuwa mamlaka nchini Gambia zilikuwa zinapanga kumdhuru yeye pamoja na timu yake" alisema mwanafamilia huyo.

"Baadhi ya wafanyakazi wake nao wamekimbilia Senegal," hata hivyo mwanafamilia huyu ambaye hakutaka jina lake lifahamike, hakueleza namna Njie alivyofanikiwa kutoroka nchini mwake.

Hata hivyo mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na mamlaka za senegal kuthibitisha ama kukanusha taarifa hizi.

Njie alimtangaza kiongozi wa upinzani Adama Barrow kuwa mshindi wa uchaguzi wa Desemba Mosi mwaka jana, na kutoa wito kwa pande zote kuheshimu matokeo hayo.

Hata hivyo punde baada ya kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo, rais Jammeh akatangaza kutoyatambua matokeo na chama chake kufungua kesi katika mahakama kuu ikitaka zoezi la uchaguzi kurudiwa.

Jammeh mwenyewe amesema anasubiri uamuzi wa mahakama kuu ambayo imechelewesha kutoa uamuzi wake hadi Januari 10 mwaka huu.

Uamuzi wa rais Jammeh kukataa kutambua matokeo ya uchaguzi huo, kumeibusha ukosolewaji mkubwa wa Serikali yake na yeye mwenyewe, hali iliyowafanya wakuu wa jumuiya ya ECOWAS kutangaza kuunda kikosi maalumu cha jeshi kitakachoongozwa na Senegal, kuingia nchini humo kumuondoa kwa nguvu ikiwa ataendelea na msimamo wake.

Taarifa kutoka nchini Gambia zinasema kuwa, watu kadhaa wamekamatwa na vyombo vya usalama baada ya kubainika wamechapisha fulana zilizoandikwa #GambiaImeamua lakini hata hivyo wameripotiwa kuachiwa.