GHANA

Nana Akufo-Addo aapishwa kuwa rais mpya wa Ghana

Nana Akufo-Addo ameapishwa kuwa rais wa Ghana, katika sherehe zilizohudhuriwa na marais zaidi ya 10 kutoka barani Afrika na maelfu ya wananchi wa nchi hiyo jijini Accra.

Nana Akufo-Addo akiapishwa
Nana Akufo-Addo akiapishwa Reuters
Matangazo ya kibiashara

Rais huyo mpya mwenye umri wa miaka 72 na Wakili wa Haki za Binadamu, amewaambia wananchi wa Ghana kuwa hatawaangusha na kazi yake kubwa itakuwa ni kupambana na ufisadi na kuinua uchumi wa taifa hilo.

“Nanyenyekea sana kwa namna ambavyo raia wa Ghana wameniamini, mimi na chama changu,”.

“Nitatekeleza majukumu yangu kwa moyo wangu wote, ili kufanya kazi mliyonipa, sitawaangusha nyinyi wananchi wa Ghana,” alisisita rais Addo.

Akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni, rais Nana amesema raia wa Ghana hawatapata tena sababu ya kuwa masikini, lakini pia amewahimiza kuwa wananchi wanaowajibika.

Rais Nana Addo anamrithi John Dramani Mahama aliyeshindwa katika Uchaguzi wa mwezi Desenba mwaka uliopita, na sasa anaongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka minne ijayo.

Katika hatua nyingine, akizungumza katika sherehe hizo rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ambaye ni Mwenyekiti wa nchi za kiuchumi za Afrika Magharibi ECOWAS, amesema muungano huo unafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Gambia wakati huu Mahakama ikitarajiwa kuanza kusikiliza kesi iliyowasilishwa na rais Yahya Jammeh kupinga ushindi wa Adama Barrow.

ECOWAS imesema itasimama na kuheshimu uamuzi wa wananchi wa Gambia wa kumchagua rais mteule Barrow na kumtaka rais Jammeh kuondoka madarakani.