GAMBIA-SIASA

Waziri wa rais Jammeh, aliyekimbilia Senegal amtambua Adama Barrow

Rais  Yahya Jammeh
Rais Yahya Jammeh Screen grab/The Gambia Enquirer

Aliyekuwa Waziri wa Habari nchini Gambia, aliyejiuzulu na kukimbilia nchini Senegal Sheriff Bojang, ametangaza kumuunga mkono Adama Barrow aliyetangazwa mshindi halali wa Uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Waziri huyo wa zamani amesema amefikia uamuzi huo baada ya kusutwa na nafasi yake kutokana na kauli ya Jammeh kusema kuwa hataachia madaraka.

Aidha, amesema kuwa haamini kuwa Mahakama ya Juu itatoa uamuzi sahihi baada ya Jammeh, kuwasilisha kesi ya kutaka Uchaguzi huo kufutwa kwa madai kuwa uligubikwa na wizi wa kura.

Marais watatu wa nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kuzuru Gambia wiki hii, kuendeleza shinikizo za kumtaka Jammeh kuondoka madarakani kabla ya tarehe 19, siku ambayo muda wake wa kukaa madarakani utafika mwisho.

Umoja wa Mataifa, Mataifa ya Magharibi na Umoja wa Afrika, umemtaka Jammeh ambaye ameongoza nchi hiyo kwa miaka 22 kuheshimu haki za raia wa Gambia na kukubali kuondoka madarakani.