Jawari achaguliwa tena Spika wa bunge nchini Somalia
Imechapishwa:
Mohamed Osman Jawari amechaguliwa tena kuwa spika wa bunge la Somalia.
Uchaguzi huo ulifanyika katika majengo ya Bunge mjini Mogadishu siku ya Jumatano, chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika AMISOM.
Kati ya wabunge 259 waliopiga kura, wabunge 141 walimchagua Jawari kuendelea kuongoza bunge kwa mara nyingine.
Kuchaguliwa kwa spika huyu mwenye umri wa miaka 71 kutoka koo ya Digil na Mirifile, kunamaanisha kuwa mwanasiasa Sharif Hassan Sheikh Adan, ambaye anatoka naye katika koo hiyo atajiondoa katika orodha ya kuwania urais.
Kuchaguliwa kwa spika na kuapishwa kwa wabunge, kunatoa nafasi kwa wabunge sasa kumchagua rais wa nchi hiyo ambayo bado inakabiliwa na changamoto za kiusalama kutokana na kuwepo kwa kundi la kigaidi la Al Shabab.
Miongoni mwa wale wanaowania urais ni pamoja na rais wa sasa Hassan Sheikh Mohamud, rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, Waziri Mkuu wa sasa Omar Abdirashid Ali Shamarke, na Waziri Mkuu wa zamani Mohamed Abdullahi Mohamed 'Farmajo'.
Somalia haijawa na serikali dhabiti tangu 1991, baada ya kuangushwa kwa utawala wa Siad Barre na jeshi la nchi hiyo, na kuzua mzozo wa kisiasa nchini humo hadi leo hii.