DRC-SIASA

DRC: Roger Lumbala awa mwanasiasa wa kwanza kunufaika na makubaliano ya Desemba 31

Mwanasiasa wa upinzani wa DRC aliyekuwa anaishi uhamishoni, Roger Lumbala.
Mwanasiasa wa upinzani wa DRC aliyekuwa anaishi uhamishoni, Roger Lumbala. Screensot/youtube

Kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa uhaini, amerejea jijini Kinshasa mwishoni mwa juma, ikiwa ni wiki mbili zimepita toka kufikiwa kwa makubaliano muhimu ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Roger Lumbala, kiongozi wa chama kidogo cha upinzani cha Rally of Congolese Democrats and Nationalists (RCD-N), alikuwa miongoni mwa watu wachache waliokuwa wakituhumiwa kwa uhaini, na kurejea kwake nyumbani kumetokana na makubaliano ya tarehe mosi ya mwezi huu.

Lumbala, ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo, alirejea jijini Kinshasa na shirika la ndege la Ethiopia, na hii ni kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa shirika la Ufaransa, AFP.

Baada ya kushindwa katika jaribio la kuwania urais mwaka 2006, Lumbala alishuhudia ubunge wake ukifutwa Januari 2013 kutokana na yeye mwenyewe kutokuwepo nchini, akidaiwa kuwa muda mwingi alikuwa nchini Uganda na Rwanda.

Mamlaka nchini DRC ilimtuhumu Lumbala kwa makosa ya uhaini na kushirikiana na kundi la M23, kundi ambalo lilizidiwa na kufurushwa mwaka 2013, kufuatia operesheni ya vikosi vya Serikali na vile vya umoja wa Mataifa.

Mbali na mazungumzo yaliyofanikisha makubaliano ya Desemba 31 mwaka jana, upande wa upinzani ukiongozwa na Etienne Tshisekedi, ulitaka kuachiwa huru kwa wafungwa wa kisiasa na kusamehewe kwa zaidi ya wanaisasa saba mashuhuri nchini humo.

Pande zote zilikubaliana kuachiwa kwa wafungwa hao wa kisiasa wanaoishi uhamishoni akiwemo Lumbala, ambaye anakuwa wa kwanza kunufaika na msamaha huo.

Ijumaa ya wiki iliyopita, baraza la maaskofu nchini DRC, walieleza kuguswa na namna ambavyo kumekuwa na ucheleweshaji wa kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa kama ambavyo ilikubwaliwa kwenye mkataba wa usiku wa kuamkia mwaka mpya.