MISRI-IS-USALAMA

Misri yawapoteza polisi wake wanane

Polisi wanane wa Misri waliuawa Jumatatu usiku katika shambulizi dhidi ya kituo cha ukaguzi. Shambulizi hili lilitekelezwa na kundi la watu wenye silaha katika jimbo la el-Wadi el-Gedid kusini-magharibi mwa Misri, wizara ya mambo ya ndani imesema.

Vikosi vya usalama baada ya shambulio la bomu katia eneo la Talibiya karibu na mji wa Cairo, Desemba 9, 2016.
Vikosi vya usalama baada ya shambulio la bomu katia eneo la Talibiya karibu na mji wa Cairo, Desemba 9, 2016. AFP
Matangazo ya kibiashara

Wawili kati ya washambuliaji waliuawa wakati ambapo polisi wengine watatu walijeruhiwa, chanzo hicho kimebainisha.

Shambulizi hili lilitokea katika kituo cha ukaguzi cha Al-Naqab, kilomita 80 kutoka mji wa El Kharga, mji mkuu wa jimbo hilo, wizara ya mambo ya ndani imeongeza.

Wanajihadi, hasa wa kundi la Islamic State wameua mamia ya askari na polisi tangu jeshi la Misri kumtimua madarakani rais Mohamed Morsi mwaka 2013. Operesheni ya kamata kamata dhidi ya wafuasi wa Morsi ilifuatia baada ya mapinduzi hayo.

Mashambulizi mengi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislam yalitokea kaskazini mwa eneo la Sinai, eneo linalopakana na Israel na Ukanda wa Gaza. Pia mashambulizi yalitokea katika maeneo mengine ya nchi, ikiwa ni pamoja na mjini Cairo.