NIGERIA-GAMBIA-USALAMA

Nigeria yatuma meli ya kivita nchini Gambia

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari aliteuliwa kuwa mpatanishi katika mgogoro wa Gambia na wenzake wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika, ECOWAS.
Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari aliteuliwa kuwa mpatanishi katika mgogoro wa Gambia na wenzake wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika, ECOWAS. Getty Images

Nigeria imepeleka meli yake ya kivita inayoitwa "NNS Unit" katika maandalizi kwa ajili ya uwezekano wa kuingilia kijeshi nchini Gambia. Chanzo cha kijeshi cha Nigeria kimesema kuwa meli ya kivita sasa inasafiri katika pwani ya Ghana kuelekea Gambia.

Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa kijeshi wa nchi za Afrika Magharibi walikutana kujadili mpango wa kupeleka kikosi cha kijeshi nchini Gambia.

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari aliteuliwa na wenzake wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, kuwa mpatanishi katika mgogoro wa Gambia.

Senegal, nchi jirani ya Gambia itaongoza uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi ya kikanda.

Pia inaandaa askari wake wa ardhini.

Jumatatu wiki hii kiongozi wa Mahakama Kuu, Emmanuel Fagbenle, alijiondoa katika kikao cha kutathmini rufaa iliyowasilishwa mbele ya mahakama na rais anayemaliza muda wake Yahya Jammeh dhidi ya kuapishwa kwa mrithi wake aliyechaguliwa Adama Barrow, tarehe 19 Januari.

Gambia imetumbukia katika mgogoro mkubwa tangu Jammeh alipotangaza Desemba 8 kuwa hatambui matokeo ya uchaguzi wa urais wa Desemba 1, wiki moja baada ya kumpongeza Bw Barrow kwa ushindi wake.