GAMBIA-ECOWAS-SIASA

Wananchi wa Gambia wamsubiri rais wao mpya

Rais Adama Barrow mjini Dakar, Januari 20, 2017.
Rais Adama Barrow mjini Dakar, Januari 20, 2017. REUTERS/Sophia Shadid

Wananchi wa Gambia wamekua wakisubiri Jumapili hii kuwasili kwa rais mpya Adama Barrow baada ya rais anayemaliza muda wake Yahya Jammeh kukimbilia uhamishoni. Yahaya Jammeh amelazimika kukimbilia uhamishoni nchini Equatorial Guinea baada ya kushinikizwa na majirani zake kutoka Afrika Magharibi.

Matangazo ya kibiashara

Katika mji wa Banjul, wananchi wamekua wakiandamana kwa furaha wakisherehekea kuondoka kwa dikteta ambaye alitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 22. Kulikua na utulivu usiku wa kuamkia Jumapili hii, kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP.

Sasa, "tunamsubiri Barrow, kutoka uwanja wa ndege hadi ikulu ya rais," Babacar Jallow, mkaazi wa mji wa Banjul amelithibitishia shirika la habari la AFP. "Kabla ya hapo, tulikuwa na hofu ya kwenda nje" kwa sababu ya ukandamizaji wa utawala wa Yahya Jammeh, kwani "Mtu huyu ni muuaji," ameongeza.

Wananchi sa Gambia wamekua na furaha baada ya kuapishwa kwa Adama Barrow katika ofisi ya ubalozi wa Gambia Januari 19, 2017.
Wananchi sa Gambia wamekua na furaha baada ya kuapishwa kwa Adama Barrow katika ofisi ya ubalozi wa Gambia Januari 19, 2017. SENEGALESE PRESIDENCY / AFP

Kwa ombi la Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Adama Barrow yuko uhamishoni tangu Januari 15 katika mji wa Senegal, Dakar, ambako aliapishwa Alhamisi katika ofisi ya ubalozi wa Gambia.

Muda mfupi baada ya kuapishwa, askari wa ECOWAS waliingia katika ardhi ya Gambia. Mara tu zoezi hilo lilisitishwa kwa kutoa fursa ya mwisho katika jitihada za kumshawishi Jammen aachie ngazi.

Yahya Jammeh alikimbilia uhamishoni Jumamosi hii nchini Equatorial Guinea baada ya mazungumzo yaliyoongozwa na marais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz na wa Guinea Alpha Condé, ambao walitumwa na ECOWAS (nchi 15 wanachama wa jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na Guinea lakini hapana Mauritania).

Jammeh, mwenye umri wa miaka 51, aliondoka Banjul Jumamosi saa 03:00 usiku saa za Gambia sawa na saa 05:00 saa za Afrika ya Kati akiambatana katika ndege ya kibinasi na rais wa Guinea Alpha Condé.

Ndge hiyo ilitua katika uwanja wa ndege wa mjini Conakry na kisha iliendelea hadi katika mji wa Malabo, nchini Equatorial Guinea.

Raia wa Gambia wakiingia mitaani mjini Banjul, wakionyesha furaha yao baada ya kuapishwa kwa rais wao mpya Adama Barrow, Alhamisi, Januari 19, 2017.
Raia wa Gambia wakiingia mitaani mjini Banjul, wakionyesha furaha yao baada ya kuapishwa kwa rais wao mpya Adama Barrow, Alhamisi, Januari 19, 2017. REUTERS/Afolabi Sotunde