GAMBIA-ECOWAS-SIASA

Vikosi vya ECOWAS vinasimamia usalama Gambia, baada ya Jammeh kuondoka

Askari wa ECOWAS katika mji wa Barra, karibu na mji wa Banjul, Januari 22, 2017.
Askari wa ECOWAS katika mji wa Barra, karibu na mji wa Banjul, Januari 22, 2017. RFI / Guillaume Thibault

Nchini Gambia, siku moja baada ya rais aliyemaliza muda wake Yahya Jammeh kukimbilia uhamishoni nchini Equatorial Guinea, kikosi cha ECOWAS kinasimamia usalama ili rais aliyechaguliwa Adama Barrow ambaye yuko uhamishoni nchini Senegal aweze kurudi nchini kwa usalama. Kikosi cha ECOWAS chenye askari 7000 kiliwasili katika mji wa Banjul Jumapili jioni Januari 22.

Matangazo ya kibiashara

Askari wa tume ya Jumuiya Mataifa ya Afrika Magharibi (Micega), waliingia katika ardhi ya Gambia kupitia maeneo mawili ya mpaka kati ya Gambia na Senegal, katika mji wa Karang na mashariki katika mji wa Keur Ayib .

Kikosi cha ECOWAS kilipokelwa vizuri na askari wa Gambia pamoja na wananchi, hasa katikamji wa Farafenni, kwenye mpaka wa kaskazini.

Lengo ni kudhibitimaeneo muhimu kwa minajili ya kulindia usalama raia, lakini hasa kuwezesha Rais mteule Adama Barrow kuchukua hatamu ya uongozi mjini Banjul. Mkuu wa kikosi cha Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Magharibi (Micega) Jenerali Francois Ndiaye amesema katika taarifa yake siku ya Jumapili asubuhi.

Jumapili usiku, rais aliyechaguliwa alikua bado yupo katika mji wa Dakar. Lakini anataka kurudi haraka iwezekanavyo mjini Banjul, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya ECOWAS, Alain Marcel de Souza,huku akiongeza kuwa itabidi usalama uimarishwe vilivyo katika mji mkuu na maeneo mengine ya nchi kabla ya Rais Adama Barrow kurudi nchini.

Jammeh akimbia na mamilioni ya fedha

Mshauri maalumu wa Rais wa Gambia Adama Barrow amesema zaidi ya dola za Kimarekani milioni 11 zinaaminika kutoweka katika hazina ya serikali, kufuatia kuondoka madarakani kwa Yahya Jammeh.

Mia Ahmad Fatty amewaambia Waandishi wa habari katika mji mkuu wa Senegal Dakar kwamba wataalamu wa masuala ya fedha wanatathmini kujua ni kiasi gani kwa sasa kimepotea.

Kwa sasa Rais Barrow amekuwa akifanya kazi na timu ya wataalamu wa masuala ya fedha na wengine kutoka Benki kuu ya nchi hiyo kupata kiasi halisi kilichopo.

Habari zinasema magari ya kifahari na mali nyingine zilionekana zikipakiwa katika ndege ya mizigo ya Chad kwa niaba ya Rais Jammeh siku alipoondoka nchini humo.