MAREKANI-SOMALIA-KENYA

Marekani yawatimua raia 92 kutoka Somalia na Kenya

Donald Trump katika kampeni zake, aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.
Donald Trump katika kampeni zake, aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani. REUTERS/Lucy Nicholson

Watu 90 kutoka Somalia na wawili kutoka Kenya wamefukuzwa nchini Marekani muda mfupi baada ya kutokea taarifa kwamba Rais Donald Trump yuko mbioni kupambana na watu wanaoishi nchini Marekani kinyume cha sheria.

Matangazo ya kibiashara

Raia hawa waliwasili katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, nchini Kenya. Raia wa Somalia wameendelea na safari hadi uwanja wa ndege wa Aden Abdulle mjini Mogadishu.

Serikali ya Kenya haijathibitishwa iwapo uamuzi wa kuwafukuza raia hao umetokana na msimamo wa rais Donald Trump,, lakini imethibitisha kufukuzwa kwa watu hao.

Bw Trump anatarajiwa kuweka masharti makali kwa raia wa mataifa saba ya Mashariki ya Kati na Afrika yenye idadi kubwa ya Waislamu wanaotafuta viza za kwenda Marekani. Awali alisema Jumatano itakuwa siku muhimu kwa usalama wa Marekani.

Donald Trump katika kampeni zake, aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.

Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi.