UFISADI

Rwanda yaongoza katika vita dhidi ya ufisadi Afrika Mashariki

Nembo ya Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi duniani  Transparency  International
Nembo ya Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi duniani Transparency International Transparency International

Rwanda inaongoza katika vita dhidi ya ufisadi kati ya mataifa 6 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Transparency International.

Matangazo ya kibiashara

Tanzania ni ya pili lakini ni ya 116 duniani, Kenya ya tatu lakini ya 145 duniani.

Rais wa Tanzania John Magufuli hivi karibuni, alizindua Mahakama maalum ya kusikiliza kesi za ufisadi, huku Kenya ikizindua tena Mahakama kama hiyo ambayo imeonekana kutofanya kazi vizuri miaka iliyopita.

Uganda inashikilia nafasi ya nne na ya 115 huku Burundi ikiwa ya nne na ya 159 huku Sudan Kusini ikiwa ya mwisho na ya 175 duniani.

Somalia inasalia kuwa taifa fisadi zaidi duniani, ikifuatwa na Sudan Kusini, Korea Kaskazini, Syria na Libya.

Bostwana inaongoza barani Afrika kwa taifa linalopambana vilivyo  na ufisadi, ikifuatwa na Cape Verde, Mauritius na Rwanda.

Hata hivyo, mataifa yanayofanya vizuri katika vita dhidi ya ufisadi ni pamoja na Denmark ambayo inaongoza, ikifutawa na New Zealand, Finland, Sweden, Switzerland, Norway, Singapore, Uholanzi Canada na Ujerumani.

Transparency International inasema mataifa mengi yanashindwa kupambana na ufisadi kutokana taasisi zilizopewa jukumu hilo kutowajibika ipasavyo.

Mwaka uliopita rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliishtumu taasisi za kupambana na ufisaidi nchini humo kwa kushindwa kufanikisha vita hivi.

Suala hili limeungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International nchini humo Samwel Kimeu ambaye pia amesema Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma pia inachelewesha uchunguzi wa kesi za ufisadi.

Ripoti hii inakuja wakati huu Tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya ikipata Mkurugenzi Mkuu mpya, Aksofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Anglikana nchini humo Eliud Wabukala.