SOMALIA-USALAMA

Shambulizi nchini Somalia: idadi ya vifo yaongezeka na kufikia 28

Watu waendelea kuangamia katika mashambulizi mbalimbali mcjini Mogadishu, nchini Somalia.
Watu waendelea kuangamia katika mashambulizi mbalimbali mcjini Mogadishu, nchini Somalia. Mohamed ABDIWAHAB / AFP

Watu zaidi ya 26 wameuawa katika shambulizi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Serikali imethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo katika hoteli moja inayofahamika kama Dayah, ambayo pia inawapa hifadhi watu mashuhuri kama wabunge.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo chanzo cha hospitali kinabaini kwamba idadi ya vifo imeongezeka na kufikia 28 na watu 43 waliojeruhiwa.

Polisi wanasema, shambulizi hilo lilitokea baada ya magari mawili madogo yaliyokuwa yamebeba mabomu na vilipuzi kulipuka mbele ya hoteli hiyo.

Waziri wa usalama nchini humo Abdirizak Omar Mohamed amesema washambulizi wanne waliotekeleza waliokuwa ndani ya magari hayo wameuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa usalama.

Aidha, polisi inasema kuwa imefanikiwa kudhibiti jengo hilo na kuwaokoa watu wengine waliokuwa ndani ya hoteli hiyo ambayo inakaribia na makaazi ya rais.

Kundi la kigaidi la Al Shabab limesema ndilo lililotekeleza shambulizi hilo.

Hii ndio mara ya kwanza kwa mwaka 2017 kwa Al Shabab kutekeleza shambulizi katika hoteli maarufu mjini Mogadishu.

Mwezi Desemba mwaka 2016, zaidi ya watu 20 walipoteza maisha baada ya Lori lililokuwa limebeba mabomu na vilipuzi kulipuka karibu na kambi ya kijeshi mjini Mogadishu.