Rais wa Gambia Adama Barrow awasili mjini Banjul
Rais mpya wa Gambia Adama Barrow amewasili mjini Banjul Alhamisi alaasiri akitokea mjini Dakar nchini Senegal ambako alikua akiishi uhamishoni tangu wiki mbili zilizopita. Umati wa watu wamekusanyika karibu na uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Gambia kwa kumlaki.
Imechapishwa:
Rais mpya wa nchi ya Gambia aliapishwa tarehe 20 Januari katika mji mkuu wa Senegal kwa sababu za kiusalama nchini mwake, baada ya rais aliyelazimishwa kuondoka nchini humo Yahya Jammeh kupinga kuachia ngazi.
Rais Adama Barrow aliomba kuendelea kwa operesheni ya kikosi cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) nchini mwake, iliozindua Januari 19 kwa minajili ya kumlazimisha Yahya Jammeh kuondoka madarakani, na kusem akuwa mazingira ya kiusalama hayatoshi kwa kurejea nchini.
Itakumbukwa kwamba Rais Yahya Jammeh aliondoka nchini Gambia Januari 21 jioni baada ya timu ya usuluhishi kujaribu mara kadhaa kumshawishi bila mafanikio.
Bw Barrow ameomba majeshi ya ECOWAS kusalia nchini Gambia kwa muda wa miezi sita ili kusaidia jeshi la Gambia kujipanga sawa na kurejesha hali ya utulivu baada ya miaka 22 ya utawala wa Yahya Jammeh.