SOMALIA

Changamoto zinazomsubiri rais ajaye wa Somalia

Majengo mapya yaliyojenga mjini Mogadishu
Majengo mapya yaliyojenga mjini Mogadishu CC/Wikimedia

Rais ajaye wa Somalia, anatarajiwa kukabiliana na changamoto za kiuchumi, ugaidi, mivutano ya kisiasa kati ya koo mbalimbali na uhaba wa chakula katika nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Uchumi wa taifa la Somalia, umeendelea kuyumba hasa kwa sababu ya ukosefu wa uwekezaji na serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha kidogo inachopata katika maswala ya usalama kwa msaada wa nchi za nje.

Pamoja na hilo, ufisadi nchini humo umesababisha uchumi kushuka kwa kiwango kikubwa kutokana na kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Ripoti ya mwaka uliopita iliyotolewa na Shirika la Transparency International, ilieleza kuwa Somalia ndio nchi inayoongoza kwa ufisadi duniani.

Sababu kubwa inayosababisha hili ni nchi hiyo iliyo kwenye eneo la pembe ya Afrika, kukosa taasisi za kukabiliana na tatizo hili.

Uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwaka uliopita, uliripotiwa kukabiliwa pakubwa na utoaji rushwa,madai ambayo pia yameripotiwa katika kampeni ya urais.

Pamoja na hilo, suala lingine ambalo limeifanya Somalia kuendelea kuwa katika hali hii ni uwepo wa kundi la kigaidi la Al Shabab.

Tangu mwaka 2006, kundi hili ambalo kwa sasa linashirikiana na Islamic State, limeendeleza mashambulizi ya kigaidi mjini Mogadishu kujaribu kuiangusha serikali inayotambuliwa Kimataifa.

Kiongozi mpya atakuwa na kibarua cha kuhakikisha kuwa kwa usaidizi wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika AMISOM, analimaliza kundi hilo ambalo linakadiriwa kuwa na wafuasi kati ya 7,000-9,000 ndani na nje ya nchi.

Ugaidi nchini Somalia umesababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia nchini Kenya na nchi zingine.

Mambo muhimu kuhusu Somalia:-

  • Idadi ya raia wa Somalia ni Milioni 12.3.
  • Asilimia 85 ya raia wa nchi hiyo ni kutoka kabila ka Kisomali.
  • Lugha za taifa ni Kisomali na Kiarabu.
  • Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo ni Waislamu, wengi kutoka Sunni.
  • Mji Mkuu ni Mogadishu.
  • Rais wengi wa Somalia ni wafugaji.