DRC

DRC yakubali kuchunguza madai ya wanajeshi wake kuwauwa watu jimboni Kasai

Mkanda wa video ukionesha namna raia walivyopigwa risasi katika jimbo la Kasai nchini DRC
Mkanda wa video ukionesha namna raia walivyopigwa risasi katika jimbo la Kasai nchini DRC Capture d'écran

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imekubali kuchunguza mkanda wa video uliowaonesha wanajeshi wa serikali wakiwafwatulia risasi na kuwauwa watu ambao hawakuwa na silaha katika jimbo la Kasai ya Kati.

Matangazo ya kibiashara

Kinshasa imetangaza kuwa, Tume maalum itakayoundwa na wanajeshi itachunguza madai ya jeshi la serikali kuhusika na mauaji hayo katika kanda iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ili kufahamu ukweli.

Serikali ya DRC imekuwa ikipata shinikizo kubwa kutoka kwa Marekani, Ufaransa, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuchunguza kuhusika kwa jeshi la serikali.

Kabla ya kukubali kuchunguza mkanda huo serikali ya DRC ilidai kuwa mkanda huo ulifanyiwa ukarabatiwa ili kulipaka tope jeshi la serikali.

Mbali na hilo, kuna wasiwasi wa kurejea kwa waasi wa zamani wa M 23 katika jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jeshi la kulinda amani nchini humo MONUSCO limesema kuwa viashiria vinaonesha wazi kuwepo kwa waasi hao wa zamani baada ya kuanza kuwashambulia wakaazi wa wilaya ya Rutshuru na kusababisha mamia ya watu kuyakimbia makwao.