AFRIKA KUSINI-ICC

Pigo kwa Afrika Kusini kuhusu mchakato wa kujiondoa ICC

Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC.
Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC. REUTERS/Jerry Lampen/File Photo

Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imesema hatua ya serikali nchini humo kutangaza kuwa inajiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu ni pigo kwa rais Jacob Zuma lakini habari njema kwa wanaharakati na wanasiasa wa chama cha upinzani cha DA waliokwenda Mahakamani kupinga hatua hiyo ya serikali.

Mahakama sasa inaitaka serikali kuachana na mpango wake wa kujiondoa kwenye Mahakama hiyo yenye makao yake jijini Hague nchini Uholanzi.

Tofauti kati ya Afrika Kusini na Mahakama ya ICC zilianza kushuhudiwa mwaka 2015 baada ya Mahakama nchini humo kuamuru kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar Al Bashir aliyekuwa nchini humo kuhudhuri mkutano wa Umoja wa Afrika, lakini Pretoria ikakataa kutekeleza agizo hilo.

Msemaji wa Wizara ya Haki Mthunzi Mhaga amesema serikali inathathmini uamuzi huo na itaamua ikiwa itakata rufaa au la.

Burundi ni nchi nyingine ya bara Afrika ambayo imentangaza kujiondoa katika Mahakama hiyo kwa madai kuwa inawaonea viongozi wa Afrika.

Hata hivyo, uongozi mpya wa Gambia umesema taifa hilo litaendelea kuwa katika Mahakama hiyo.

Kenya pia imewahi kusema inataka kujiondoa kwenye Mahakama hiyo huku Uganda nayo kupitia kwa rais Yoweri Museveni akisema Mahakama hiyo haina maana.