SOMALIA

Rais mpya wa Somalia atawazwa rasmi, aahidi kupambana na Al Shabab

Wanawake nchini Somalia wakiwa wanasherekea ushindi wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed, mjini Mogadishu
Wanawake nchini Somalia wakiwa wanasherekea ushindi wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed, mjini Mogadishu REUTERS/Feisal Omar

Mohamed Abdullahi Mohamed anayefahamika kwa jina maarufu la Farmajo, ametawazwa rasmi kuwa rais wa Somalia baada ya kushinda Uchaguzi wa urais wiki mbili zilizopita.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa ndege jijini Mogadishu chini ya ulinzi mkali kwa hofu ya kutokea kwa shambulizi kutoka kwa magaidi wa Al Shabab, huku barabara na maduka yakifungwa.

Rais Farmojo mwenye umri wa miaka 54, anakuwa rais wa tisa wa nchi hiyo ambayo imekuwa katika changamoto za kiusalama kutokana na kuwepo kwa kundi la kigaidi la Al Shabab.

Katika hotuba yake, rais huyo mpya amewaonya magaidi wa Al Shabab kuwa serikali yake kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, itaendelea kupambana nao, lakini pia akawakumbusha kuwa hawawezi kuwashinda raia Milioni 12 wa Somalia.

Aidha, ameahidi kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa dhana ya kuwa nchi hiyo ndio fisadi zaidi duniani, inaondoka, kwa kuimarisha suala la uongozi bora.

Rais huyo mpya amesema kuwepo kwenye sherehe hizo  viongozi wa zamani Hassan Sheikh Mohamud na Sharif Sheikh Ahmed ni ishara ya kukomaa kwa demokrasia nchini humo.

“ Hatua ya Marais hawa wawili kusimama pembeni yangu, ni ishara ya demokrasia na huu ndio wakati wa kushindana na nchi zingine duniani,” alisema rais Framajo.

Sherehe hizi pia zilihudhuriwa na rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh na Uhuru Kenyatta kutoka Kenya pamoja na viongozi wengine mashuhuri kutoka nje ya nchi hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, rais Kenyatta amewapongeza raia wa Somalia katika jitihada za kuimarisha demokrasia lakini pia akaahidi kuwa nchi yake itaendelea kusaidia katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Kenya ni mojawapo ya nchi kutoka bara Afrika, ambayo imetuma wanajeshi wake chini ya mwavuli wa AMISOM kupambana na Al Shabab.