MOROCCO-POLISARIO

Morocco yaagiza kuondoka kwa vikosi vyake kwenye eneo la mpaka na Sahara Magharibi

Nchi ya Morocco inatarajia kujiondoa kwenye ukanda wa mpaka wenye utata na eneo la Sahara Magharibi, eneo ambalo pia lina wanajeshi wa umoja wa Mataifa wanaosimamia usalama kati ya pande hizo mbili.

Mfalme wa 6 wa Morocco, akisindikizwa na walinzi wake hivi karibuni.
Mfalme wa 6 wa Morocco, akisindikizwa na walinzi wake hivi karibuni. REUTERS/Tiksa Negeri
Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Morocco bado imeendelea kusisitiza kuwa koloni hilo la zamani la Uhispania ni sehemu ya nchi yake, lakini watu wa vuguvugu la Polisario wanataka kufanyike kwa kura ya maoni ya kujitenga kwa eneo hilo.

Sintofahamu ilitanda zaidi mwaka mmoja uliopita wakati nchi ya Morocco ilipoamua kusogea kwenye eneo huru lililotengwa na umoja wa Mataifa, hatua iliyokiuka makubaliano ya umoja wa mataifa ya usitishaji wa mapigano.

Hivi karibuni nchi ya Morocco ilirejea kwenye umoja wa Afrika baada ya kujitenga kwa sababu nchi wanachama za umoja huo ziliitambua Sahara Magharibi kama nchi huru.

Uamuzi wa nchi hiyo kujiondoa kwenye eneo lenye utata, umeelezwa ulitoka moja kwa moja kwa Mfalme Mohamed wa VI.

Hatua yake imekuja baada ya kuzungumza na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliyemuomba aondoe wanajeshi wake kwenye eneo ambalo tayari lilikubaliwa kuwa chini ya uangalizi wa umoja wa Mataifa.

Sahara Magharibi ilichukuliwa na Morocco mwaka 1975, uamuzi ambao ulipingwa na watu wa eneo hilo, ambapo kulizuka vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 16 kabla ya kusitishwa chini ya usimamizi wa umoja wa Mataifa mwaka 1991 na kuahidiwa kufanya kura ya maoni kuhusu kujitenga.